×

 Dansi Mmepewa Lifti na Babu Seya, Papii, Pigeni honi!

MUZIKI wa Dansi Bongo ulikuwa na nafasi kubwa sana, miaka sita iliyopita. Ulikuwa unapigwa kwenye kumbi mbalimbali za starehe, mashabiki walikuwa wakipanga foleni kwenda kutazama na kuinjoi maisha.

Kwa wale wafuatiliaji wa muziki huu, hakika wataungana na mimi kwamba, muziki wa dansi kwa sasa umeshuka kiwango chake cha kupendwa. Hauzungumzwi kwenye vyombo vya habari na badala yake, Bongo Fleva imeshika hatamu.

 

Viwanja vya starehe kama pale Maisha Club, Msasani Club, Leaders Club, TTC Club- Chang’ombe na kwingineko, dansi halipigwi lile la enzi zile. Ushawishi ule wa kuwateka hadi mastaa kutoka kada mbalimbali umepungua.

Mnakumbuka kipindi kile Mango Garden Kinondoni palivyokuwa panafunga wasanii wa Bongo Movies wakati The African Stars ‘Twanga Pepeta’ ilipokuwa ikifanya mambo yake jukwaani? Mnakumbuka wanasiasa wakubwa, wanamichezo walivyokuwa wanafurika pale Leaders Kinondoni?

 

Dansi ilikuwa imeshika hatamu. Kila kona ulikuwa ukizungumzwa mjadala wa nani mkali kati ya Twanga Pepeta, FM Academia, Extra Bongo, Mapacha Watatu, Malaika Music na nyinginezo. Vijana kama Chaz Baba, Muumini Mwinjuma, Chokoraa, Jose Mara, Christian Bella na wengine walikuwa juu.

Vyombo vya habari viliandika skendo zao. Stori zao zilikuwa juu kwenye vyombo vya habari na kuwafanya mashabiki waendelee kuwafuatilia. Unakumbuka Chaz Baba alivyokuwa ‘hot’ na penzi la muigizaji Wema Sepetu?

Chaz huyo huyo akawa juu na penzi la muigizaji Husna Idd ‘Sajent’. Mambo yalikuwa ni moto. Rais wa FM Academia, Nyoshi El Sadaat alikuwa habari kila siku kwenye vyombo vya habari lakini kwa sasa, chariii!

 

Anazungumzwa Diamond, AliKiba, anazungumzwa Aslay na kina Dogo Janja ambao wanafanya muziki wa Bongo Fleva. Diamond na Kiba wamefanya matusi makubwa katika maisha yao. Wana mijengo ya mamilioni, wana magari makubwa ya kutembelea, wana mtaji mkubwa wa mashabiki.

Unamzungumzia Diamond ambaye sasa ana wafuasi zaidi ya milioni 4 kwenye mtandao wa Instagram. Kiba mwenye wafuasi zaidi ya milioni 2. Dansi haina hata akauti. Wanamuziki wachache sana wa muziki wa Dansi ambao wana akaunti Instagram.

 

Wanamuziki Nguza Viking na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ walitoka kwa msamaa wa Rais, Dk John Pombe Magufuli. Mara baada ya kuingai uraiani, wameonesha kuamsha morali ya Dansi. Watu wengi wamekuwa wakiwafuatilia kwa huruma ya kufungwa gerezani

Dansi inaoonekana kuamka upya. Bahati nzuri wamekuja kisasa na kuingia Studio za Wanene Entertainment, kurekodi nyimbo zao na sasa wameanza kujiandaa kwa kupiga picha (photo shoot), kwa ajili ya promosheni za mitandao nakadhalika. Papii sasa ana akaunti Instagram ambao ndani ya muda mfupi ina wafuasi wasiopungua elfu 27.

 

Wanamuziki wa Dansi wanapaswa kuwatumia hawa kama chachu ya kuamka upya. Kutoka kwao kuwape morali ya kufanya tena vizuri. Shirikianeni nao katika nyimbo zenu. Dansi la sasa linapaswa kuwa la kisasa, jifunzeni kupitia kwa Bella.

Bella anafanya Dansi fupi lenye ujumbe ambao unachoma. Anashirikiana na wanamuziki wa Bongo Fleva. Nyimbo zake zinakuwa fupi, tamu kwa nini msifuate mfumo huo? Inashindikana nini sasa hivi kufanya kolabo na wasanii wa Bongo Fleva?

 

Watumieni kina Babu Seya kupandisha morali ya muziki. Huu ndio wakati wa kufanya nao kazi, kuzipa kasi katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Ni wakati wa kujitangaza kwa kupiga picha nzuri na kuziweka mitandaoni kutangaza kazi zenu.

Biashara yote ni matangazo na ndio maana kila siku mitandao ya simu za mkononi imekuwa ikiendelea kujitangaza. Jitangazeni kwani mkijifungia, mashabiki ndio wanatawasahau kabisa na mwisho wa siku itakuwa ndio kaburi lenu.

NA ERICK EVARIST | AMANI