
HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite, amegoma kujitoa katika kusikiliza kesi inayowakabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel.
Awali leo januari 25, Sugu na Masonga kupitia mawakili wao waliwasilisha hoja mahakamani hapo ya kumkataa hakimu huyo kwa madai kuwa hawana imani naye ambapo hakimu alikataa kujitoa akisema hoja zilizowasilishwa hazimfayi ajiengue kuendesha kesi hiyo.
Baada ya Mteite kukataa kujitoa kusikiliza kesi hiyo, mawakili wa upande wa utetezi (mawakili wa Sugu na masonga) wamejiengua katika kuendelea na kesi hiyo.
Watuhumiwa wameiomba mahakama kuwapa wiki mbili ili watafute mawakili wengine ambapo hakimu ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 2, mwaka huu.
Sugu na Masonga wanatuhumiwa kutumia maneno ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli katika mkutano wao wa hadhara na wananchi walioufanya Desemba 30, mwaka jana.