×

Simba Inakutana Na Nguli Wa Afrika

MWAKA 2003, Simba ikiwa na kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji vijana na wazoefu ilifanikiwa kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini safari yao haikuwa nyepesi.

 

Katika hatua ya awali Simba iliitoa Botswana Defence Force XI ya Botswana, Raundi ya Kwanza ikaitoa Santos ya Afrika Kusini. Baada ya hapo ikakutana na Zamalek ya Misri ambao ndiyo walikuwa mabingwa watetezi.

 

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawassa anasimulia kwa ufupi juu ya mchezaji aliyekuwa staa wa Zamalek, Hossam Hassan.

Pawassa anasema: “Kipindi hicho ndiyo Zamalek ilikuwa imetoka kupewa ubingwa, tukapangwa kukutana nao katika Raundi ya Pili ambayo ni ya mtoano kabla ya kuingia Hatua ya Makundi.

 

“Kwanza kabla ya kuelekea mchezo huo tulipewa presha kubwa sana kwa kuwa Zamalek walikuwa katika ubora wa juu, nakumbuka kabla ya mchezo huo nilipata takribani SMS zaidi ya 250, lakini nyingi kati ya hizo zilikuwa ni kuhusu Hossam Hassan.

 

“Niliambiwa naenda kukutana na mchezaji bora wa michuano ya Afrika pia alikuwa mfungaji bora wa michuano ya Mataifa ya Afrika.

“Sikuwahi kuwa na majukumu mazito kama niliyopewa kuelekea mchezo huo. Nashukuru Mungu katika mchezo wa kwanza nilifanikiwa kumdhibiti (Hossam), ilipofika dakika ya 75 akanipiga kiwiko na kunichana juu ya jicho, nilishonwa nyuzi sita na kufanikiwa kuendelea na mchezo… Jamaa alikuwa hatari.”

Hiyo ni sehemu ya simulizi ya Pawassa, baada ya hapo Simba walifanikiwa kusonga hatua ya makundi kwa penalti kutokana na matokeo ya bao 1-1 katika michezo yote miwili.

Hossam Hassan ni nani?

Ni straika wa zamani ambaye ana heshima kubwa kwenye soka la Misri na Afrika kwa jumla. Anatarajiwa kukutana na Simba, wiki ijayo akiwa katika sura na majukumu tofauti kwa mara nyingine.

Hossam ambaye ana umri wa miaka 51 ni kocha mkuu wa Al Masry ya Misri ambayo itakipiga dhidi ya Simba katika Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Timu hizo zitakutana Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jini Dar kisha zitarudiana wiki moja na nusu baadaye nchini Misri.

Hossam ambaye enzi zake alijulikana kwa uwezo wake wa kufunga mabao, kucheza soka la nguvu na kuwa mhamasishaji anapokuwa uwanjani na hata akiwa nje ya uwanja, ndiye mtu maarufu zaidi katika msafara huo wa Al Masry utakaotua nchini.

 

Licha ya kuwa staa wa timu ya taifa ya Misri na Zamalek, kabla ya hapo aliwahi kuichezea Al-Ahly ambao ni wapinzani wakubwa wa Zamalek.

Kocha huyo mkongwe pia aliwahi kuichezea timu anayoifundisha sasa katika vipindi viwili japokuwa hakuwa na mafanikio makubwa katika kikosi hicho.

Mara baada ya kustaafu kucheza soka mwaka 2007 aliamua kuelekeza nguvu zake kwenye ukocha na moja kwa moja akaanza na Al- Masry mwaka 2008.

 

Baada ya hapo akawa anahama timu moja kwenda nyingine, timu alizozifundisha ni Telecom Egypt (2009), Zamalek (2009-2011) na Ismaily (2011).

 

Mwaka 2012 alirejea Al-Masry hakudumu muda mrefu, miezi 12 baadaye yaani mwaka 2013 akatua Misr El-Makasa, Jordan (2013– 2014), Zamalek SC (2014) na Al- Ittihad Alexandria (2014–2015). Kuanzia mwaka 2015 ndipo alipoamua kurejea Al Masry, amb-apo ndipo alipo hadi sasa.

Hadi sasa anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika timu ya taifa ya Misri, akiwa amefunga mabao 69 katika mechi 169.

Ana hasira za karibu

Akiwa mchezaji alikuwa ni mtu mwenye hasira za karibu na mara kadhaa aliingia kwenye utata na wapinzani, ndiyo maana hata kwa Pawassa alipoona ‘dogo anamzingua’ akamtandika ‘kipepsi’.

Aliiwakilisha nchi yake katika Kombe la Dunia 1990 pamoja na kucheza michuano saba ya Kombe la Afrika (Afcon), lakini pamoja na sifa hizo siyo mnyonge hata sasa akiona anaonewa au mtu anamfanyia ndivyo sivyo.

Anusurika kwenda jela

Aliwahi kutupwa lupango kwa siku nne baada ya kumta-ndika mpigapicha uwanjani. Tukio hilo lilitokea wakati timu yake ya Al-Masry ilipocheza dhidi ya Ghazl el-Mahalla ambapo katikati ya mchezo kukatokea kutoelewana baina ya wachezaji wa pande mbili.

Hossam akaingilia ugomvi huo, wakati akiingilia kuna mpiga picha akawa anafanya kazi yake kwa kila kitu kinachoendelea, ndipo akawaacha wachezaji na kumvaa ‘paparazi’ huyo.

Alisamehewa baada ya mpiga picha kuamua kufuta kesi siku chache baadaye lakini bado kocha huyo alifungiwa mechi tatu na kupigwa faini.

Kulipa kisasi kwa Simba

Baada ya Simba kuwafanyia kitu kiibaya Zamalek mwaka 2003, hii itakuwa nafasi kwake kulipiza kisasi kwa Simba, kwani baada ya kipindi hicho umaarufu na ubabe wa Zamalek ulipotea kwa miaka kadhaa.

Wako pacha

Hossam Hassan ana pacha wake anayeitwa, Ibrahim Hassan ambaye pia alikuwa mchezaji wa soka, enzi zake alikuwa beki wa kulia. Kwa sasa wapo pamoja ndani ya Al Masry lakini Hassan ni Mkurugenzi wa Ufundi, wanafanana sana na ukiwa hauko makini unaweza kuwachanganya.

JOHN JOSEPH, Dar es Salaam