
BAADA ya kutamba katika kiungo, Yanga sasa imeisuka upya safu yake ya ulinzi ikimshirikisha Papy Kabamba Tshishimbi, Kelvin Yondani na Andrew Vincent ‘Dante’ ili isiruhusu bao kirahisi.
Kocha wa Yanga, George Lwandamina hataki timu yake iruhusu mabao yasiyoeleweka hivyo ameamua kumshirikisha Tshishimbi katika ulinzi akishirikiana na Yondani na Dante ambao ni mabeki wa kati.

Katika mazoezi ya mwisho ya Yanga jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Singida ambako leo wanacheza dhidi ya Singida United mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Namfua, Lwandamina alionekana akiitengeneza kombinesheni hiyo ya ulinzi.
Akiisuka safu hiyo ya ulinzi, kocha huyo pia aliwajumuisha mabeki wa pembeni Hassan Kessy na Gadiel Michael.
Lwandamina alionekana akiwapa mazoezi ya jinsi ya kuzuia na kupunguza mashambulizi wakati timu inashambuliwa huku akimpa maelekezo Tshishimbi ya jinsi ya kuanza kuzuia mashambulizi.
Tshishimbi alipewa maelekezo ya kuzuia kuanzia katika eneo lake la kati kabla ya wapinzani kufika kwa mabeki wa kati ambao ni Yondani na Dante.
Kocha huyo, pia alionekana akiwapa wachezaji hao mbinu ya jinsi ya kuanzisha mashambulizi kwa kuondoka kwa pamoja langoni kwao huku akimtumia Tshishimbi kupeleka mipira kwenye lango la wapinzani.
Hadi sasa Yanga imefunga mabao 11 katika ligi kuu huku ikiruhusu mabao manne wakati Simba ikiwa na mabao 20 na imeruhusu mabao matano, lakini Mtibwa Sugar yenyewe mabao matatu lakini Azam FC imeruhusu mabao mawili tu katika mechi nane.
Stori: Wilbert Molandi na Musa Mateja | Global Publishers