×

Pugu Wampongeza Meya Dar Kwa Huduma ya Maji  

 

Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (mwenye suti nyeusi) akitoa maelekezo kwa Diwani wa Kata ya Pugu, Bonivesture Mphuru na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mustafa, Bahati Lusizi, leo alipotembelea na kukagua mradi wa maji kwenye kata hiyo, ambapo kwa sasa wananchi hao wameanza kupata maji safi na salama.
…Akimtwisha mwananchi ndoo ya maji huku akishuhudiwa na madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
...Wakinyanyua ndo ya maji.
Mwita akizungumza jambo.
…Akiwa madiwani wa jiji  leo walipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya kilomita 0.7 kuingia katika Dampo la Pugu Kinyamwezi inayojengwa kwa kiwango cha zege.

 

WANANCHI wa Kata ya Pugu, Mtaa wa Mustafa, wamempongeza Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita,  kwa kuwapelekea maji safi na salama wakisema ameweka historia ya kutatua changamoto waliyokuwa nayo kwa muda mrefu.

Kata hiyo ambayo inadaiwa kuongoza kwa changamoto ya maji kwa kipindi kirefu, imeweka historia hiyo leo baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa maji kupitia mabomba ya mitaani.

 

Akizungumza na wananchi hao, Mwita ameahidi pia kuongeza huduma hiyo kwenye maeneo ambayo yana changamoto ya maji katika jiji lake.

 

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mustafa, Bahati Lusizi,  alimshukuru Meya Mwita kwa juhudi alizozionyesha  hadi kufanikisha kuwapatia huduma hiyo na kuondoa kilio cha muda mrefu.

 

Amesema tangu kuingia kwa uongozi wake pamekuwa na mafanikio makubwa ambapo wameweza kupata maji baada ya maombi waliyoyatoa kwa muda mfupi tu.

 

Awali Meya Mwita akizungumza na madiwani na wananchi walioshuhudia mradi huo wa maji, amesema kuwa juhudi zilizofanyika katika eneo hilo zitatumika kwenye maeneo mengine ili kila mwananchi wa kata hiyo aweze kunufaika na kuondokana na kero hiyo.

 

Amewaelekeza viongozi wa eneo hilo kwamba ifikapo Aprili mwaka huu, wananchi  wapate huduma ya maji kwa bei ya shilingi 50 kwa kila ndoo badala ya sh.100 ambayo wanauziwa kwa sasa.

 

Wakati huo huo, Meya Mwita ameridhishwa na ujenzi wa ukuta wa Dampo la Pugu Kinyamwezi unaoendelea hivi sasa ambapo wakandarasi wanaojenga ukuta huo wamemtoa wasiwasi wa kueleza kuwa ujenzi huo hautakuwa na madhara kwa wananchi waliopo karibu na eneo hilo.