
WAKATI wapenzi na mashabiki wa Simba wakiwa bado wanajiuliza juu ya matokeo ambayo timu hiyo iliyapata Ijumaa iliyapata dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wiki hii pia itakuwa na kibarua kingine dhidi ya Al Masry ya nchini Misri.
Simba itapambana na Al Masri, Jumtano hii ya Machi 7, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Lakini pia, siku moja kabla ya mechi hiyo Yanga nayo itapambana na timu ya Township Rollers ya Botswana uwanjani hapo katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika.
Simba na Yanga kwa pamoja zitakuwa zikiipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano hiyo ya kimataifa ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mechi hizo ni muhimu sana kwa Simba na Yanga kuhakikisha zinaibuka na ushindi ili ziweze kujitengezea mazingira mazuri ya kusonga mbele katika hatua nyingine michuano hiyo.

Wachezaji wa timu hizo wanatakiwa kujipanga vilivyo ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri yatakayozipunguzia kazi katika mechi zao za marudiano.
Natambua kuwa haitakuwa kazi nyepesi lakini endapo wachezaji kwa kushirikiana na viongozi wa timu hizo watajipanga hakuna kitakachoshindikana.
Kwa upande wa timu ya Simba ambayo itapambana na Al Masry, wachezaji wa timu hiyo wanatakiwa kuwa makini zaidi kukabiliana na mbinu za Waarabu hao.
Mara nyingi timu za Kiarabu zinapokuwa ugenini huja na mikakati ya kutafura sare kwa na hutumia muda mwingi kupoteza muda ili kuhakikisha wapinzani wao hawapati ushindi mkubwa.
Kwa hiyo, wachezaji wa Simba wanapaswa kulitambua hilo na kuingia uwanjani kwa kazi moja tu ya kutafuta ushindi mnono lakini pia wasikubali kutekwa kiakili na kulazimishwa kucheza soka kama Waarabu hao wanavyo taka.
Kasi ambayo Simba wamekuwa wakionyesha katika mechi zao za Ligi Kuu Bara kwa kuzitungua baadhi ya timu mabao mengi ndiyo wanayopaswa kuonyesha katika mechi hiyo na ikiwezekana iwe zaidi ya hiyo.
Kama mwaka 2003 wachezaji wenzao waliokuwa wakiunda kikosi cha timu hiyo walifanikiwa kuitupa nje ya michuano Klabu Bingwa Afrika timu ya Zamalek ambayo ilikuwa bingwa mtetezi wa michuano hiyo, kwa nini wao washindwe.
Inawabidi nao waonyeshe ubora wao kwa kuifunga Al Masry ambayo rekodi yake katika michuano ya kimataifa haitishi sana kama ilivyoliwa kwa Zamalek, lakini pia hata katika ligi lii ya nchi hiyo matokeo yake hayatishi sana.
Katika ligi ya Misri timu hiyo inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 48 wakati timu inayoongoza ligi hiyo ambayo ni Al Ahly ina pointi 72.
Kutokana na hali hiyo, wachezaji wa Simba wakiingia uwanjani kwa kazi moja tu ya kupambana kuhakikisha wanapata ushindi mnono inawezekana kabisa.
Kwa upande wa Yanga, nao jukumu ni lilelile tu la kupambana vilivyo uwanjani kuhakikisha wanapata ushindi.
Hakuna, jambo jingine ambalo linaweza kuwasaidia ila kupamba kama ambavyo wamekuwa wakipambana katika mechi zao za hivi karibuni katika michuano ya ligi kuu.
Wachezaji watakaopata nafasi ya kuitumikia Yanga katika mechi hiyo kila mmoja anatakiwa kupambana kwa nguvu zote huku akijua kuwa maelfu ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo wanamtegemea yeye ili kuwapatia furaha.
Kasi ile ambayo walianza nayo walipocheza dhidi ya St Louis wanatakiwa iongezeke zaidi kwani timu wanayokutana nayo ni nzuri na imefanikiwa kutinga katika hatua hiyo baada ya kuifunga moja ya timu kubwa Afrika.
Township Rollers imeweza kutinga katika hatua hiyo baada ya kuitupa nje ya michuano hiyo timu ya El Merrekh ya Sudan.
Lakini pia katika Ligi Kuu ya Botswana, timu hiyo ndiyo inayoongoza msimamo wa ligi hiyo, kwa hiyo ni timu mzuri hivyo wachezaji wa Yanga wanatakiwa kupambana kwelikweli.
Kwa kumalizia mimi pamoja wa Watanzania wengine tunaopenda soka tutajitokeza kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kuwaunga mkono wachezaji hao wa Simba na Yanga, nawaomba wasituangushe.