





IKAO cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam (RCC) kimepongeza kazi inayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika kushughulikia kero za wananchi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, ulinzi, usalama na sekta nyinginezo.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amesema Mkoa wa Dar es Salaam umepiga hatua kubwa kwenye maboresho ya sekta ya afya kupitia ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto Hospitali ya Amana, Hospital ya Mama na Mtoto Chanika, Jengo la Upasuaji kwa Wajawazito Hospitali ya Mwananyamala na jengo la wagonjwa wa dharura Hospitali ya Temeke, zote zikiwa ni jitihada binafsi za Makonda.
Aidha Bi. Mjema amesema kwenye sekta ya elimu, mkoa umeendelea kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa na sasa Makonda yupo kwenye kampeni ya ujenzi wa ofisi 402 za walimu, kazi yote hiyo ikiwa ni kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu.
Aidha Mjema amesema licha ya kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya awamu ya tano, bado zipo changamoto mbalimbali zinazokabili mkoa huo ukiwemo ujenzi holela, biashara holela, ombaomba, watoto wa mtaani na uchafuzi wa mazingira ambapo tayari Makonda ameshaagiza kila halmashauri itenge fedha za ununuzi wa mitambo ya usafishaji wa mazingira katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017-18.
Hata hivyo, Mjema amesema mkoa umeweza kuwatambua watumiaji wa madawa ya kulevya zaidi ya 6,000 ambapo kati ya hao 2,000 wamepatiwa ushauri wa jinsi ya kuacha madawa hayo, 1,700 wanatumia methadone, na wengine 250 wako nyumba za matibabu (sober houses), hizi zote zikiwa ni jitihada za mkuu wa mkoa huyo kuokoa nguvu-kazi za vijana zilizokuwa zikipotea kutokana na matumizi ya madawa hayo.