×

DIAMOND, DERULO KUOGELEA MAMILIONI!

Jason Derulo.

 

“HUWA najisikia kama kipepeo hivi pindi ninapotoa wimbo mpya. Lakini kwa huu wa sasa hivi najiona tofauti kabisa…” Jason Derulo akiongelea wimbo mpya wa Colors akiwa ameegemea ukuta wa Studio za Warner Bros. Records, California nchini Marekani.

 

Macho na masikio kwa mashabiki wengi ni kuusikia rasmi wimbo huo utakaotoka Machi 16 ukiwa wimbo maalum wa Coca Cola kutumika katika ufunguzi wa Kombe la Dunia linalotarajiwa kufanyika mapema Juni 14, hadi Julai 15, mwaka huu nchini Urusi.

 

Jason Derulo chini ya lebo inayomsimamia ya Warner Bros. Records imeingia makubaliano na Coca Cola kwa ajili ya kutunga wimbo huo na kuurekodi huku ukishirikisha wakali wengine kibao wa Afrika kama Diamond Platnumz kutoka Tanzania, Casper Nyovest kutoka Afrika Kusini, Sami Dani kutoka Ethiopia, Ykee Benda kutoka Uganda na Lizha James kutoka Msumbiji.

 

Diamond.

 

Watakaopafomu

 

Mara ya mwisho kwa Coca Cola kuingia makubaliano na msanii kisha kuimba wimbo wa Kombe la Dunia ilikuwa 2009 walipoingia na mkali mwenye asili ya Somalia na Canada, Keinan Abdi Warsame ‘K’naan’ ambaye alitikisa na Wimbo wa Waving Flag uliotumika katika uzinduzi wa kombe hilo uliofanyika mwaka 2010, Soweto nchini Afrika Kusini.

 

Coca Cola waliingia makubaliano na K’Naan chini ya Lebo yake ya A&M/ Octone Records na kuwapatia kiasi cha dola 150,000 (zaidi ya milioni 330 za Kitanzania) kama sehemu ya udhamini wa kutunga na kurekodi na kiasi cha dola 7,500 (Mil.16) hadi 25,000 (Mil.56) kwa kila shoo aliyokuwa akifanya K’Naa baada ya uzinduzi.

Jumla Coca Cola katika kampeni ya Kombe la Dunia kupitia wimbo huo, waligharamia dola milioni 300 (zaidi ya bilioni 600) kwenye kila kitu kuanzia matengenezo ya albamu nzima iliyojulikana kwa jina la Troubadour yenye zaidi ya lugha 20 mpaka ziara iliyofanywa nchi mbalimbali duniani pamoja na ubalozi ambapo malengo yao yalifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani albamu tu iliuza nakala zaidi ya 59,000 nchini Marekani na Canada pekee.

Casper Nyovest.

Mamilioni watakayovuna

 

 

Kama ilivyo kwa K’Naan, safari hii wameweka tena mzigo mezani wa zaidi ya bilioni 600 kwa Kampuni ya Warner Bros kuhakikisha wanampa majukumu Jason Derulo ya kutunga wimbo huo kwa kushirikiana na wakali hao kutoka nchi tofauti na kuuimba rasmi katika uzinduzi wa fainali za Kombe la Dunia 2018.

 

Inaelezwa kuwa, Diamond, Casper pamoja na wakali wengine (kasoro Jason) watanufaika kwa kuingiza mkwanja mnono kuanzia dola 30,000 (milioni 67) hadi dola 60,000 (milioni 137) ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya wimbo huo pamoja na uzinduzi.

 

Mbali na hapo, Coca Cola watashirikiana na Warner Bros. Records kutangaziwa wimbo huo sehemu kubwa ya dunia ambapo kwa kila shoo watakayopiga katika kampeni hiyo watakuwa wakiingiza kati ya milioni 50 hadi 100.

 

Sami Dani

 

Kwa nini unatumika Kombe la Dunia?

Coca Cola wakiwa sehemu ya ‘patna’ wa Kombe la Dunia, hupata nafasi ya kuandaa msanii au wasanii watakaotumbuiza katika uzinduzi na fainali.

 

Mbali na Coca Cola, kuna makampuni mengine yanayotumika kutayarisha wasanii kuimba katika uzinduzi na fainali za kombe hilo, mfano mwaka 2010 wakati Coca Cola wakim-tumia K’Naan na Wimbo wa Waving Flag, Pepsi nao walimtumia Akon pamoja na Keri Hilson katika Wimbo wa Oh Afrika huku waandaaji wakuu, FIFA wakimtumia Shakira na kundi kutoka Afrika la Freshlyground katika Wimbo wa Waka Waka (This Time For Africa).

Andrew Carlos