
Kundi la wanamuziki wa Bongo Fleva ‘Anonymous Gang’ linalotamba kwa sasa na ngoma yao ya ‘Kama Kibiti’ wamefungukia ishu inayosambaa mitandaoni kuwa wamejiita jina hilo lenye maana ya ‘Watu Wasiojulikana’ kwa sababu ya kutafuta kiki kwani hivi karibuni watu wasiojulikana wamekuwa maarufu sana kufuatia matukio mengi ya kutisha yanayotokea Bongo kudaiwa hufanywa na watu hao.
Kundi hilo linaloundwa na wanamuziki wawili Chris Nashon na Janu Rocka, wamefunguka kuwa hawategemei kiki kuendesha muziki wao, na wao kujiita Anonymous Gang haimaanishi kuwa wana uhusiano wowote na watu wanaofanya matukio hayo.

“Imezoeleka wasanii Bongo wanazingatia sana kiki kuliko kutoa ngoma kali, sisi tupo tofauti kazi kwanza hayo mambo mengine yasiyo ya lazima hatuna taimu nayo,” amesema Janu Rocka.

Akizungumzia harakati zao kimuziki Chris Nashon amesema kuwa wameshapambana sana katika gemu la muziki, milima na mabonde vyote wameshapitia lakini kwa sasa wameachia Kama Kibiti inayoendelea kufanya vizuri na wapo jikoni kupika chuma kingine kikali zaidi hivyo mashabiki wakae mkao wa kula.
NA ISRI MOHAMED