
Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) amefungua mkutano wa 11 wa Baraza hilo akiwataka Wafanyabiashara wachangie kero zao kwa uwazi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mkutano huo umewahusisha pia Mawaziri, Makatibu, Wakurugenzi pamoja na watendaji wengine wa Serikali ambao wanajibu maswali ya moja kwa moja kutoka kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Rais amesea wafanyabiashara wanaodaiwa kodi za miaka ya nyuma, wakae wajadiliane na Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wafikie mwafaka, waone kama wanaweza kuwapunguzia madeni hayo ili waweze kuyalipa.
Amehoji kwa nini Tanzania ikose kiwanda cha kuzalisha sukari ya viwandani huku akisema suala la sukari limewagharimu watu wengi ikiwemo mawaziri toka enzi za Mkapa.
Rais amesema ni viwanda nane pekee ambavyo viliagiza sukari ya kiwandani na kutumia kihalali bila udanganyifu ikiwemo SBC(Pepsi) na Bakhresa. Pia, ameelezea kuhusu serikali kufanya biashara na pesa zake na kusema serikali kutoa pesa zake benki na kutokwenda kukopa imefanya benki kuwakopesha watu wa kawaida na wafanyabiashara.

Pia, amesema ndani ya serikali na wabunge hawaoni tatizo la mafuta kuagizwa kwa sababu wakati wa Bunge, wafanyabiashara wanahamia Dodoma kufanya ‘Lobbying’ na bia kunywewa. Ametaka wanaoagiza wapigwe kodi kubwa hata mara mbili ili kuwa-discourage na wakamshtaki popote.
Amesema Tanzania hata ikikosa mafuta zitapondwa hata karanga au mafuta ya samli. Amesisitiza Tanzania inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya ajabu na mengine yamesha-expire.
Rais Magufuli amesema bajeti ya afya imepanda kutoka Bilioni 31 hadi 269 na Tanzania imepewa tenda ya ku-supply madawa katika SADC. Anasema hata Drip ya maji zimeagizwa Uganda kwa kutumia dola zaidi ya milioni 10.