×

MWIGULU MGENI RASMI TAMASHA LA PASAKA MWANZA

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.

 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Pasaka linalotarajia kufanyika Aprili Mosi mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama amesema kuwa Nchemba amethibitisha kuwa mgeni rasmi kwenye tamasha hilo.

Msama ameongeza kuwa awali mgeni rasmi alikuwa awe Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samiah Suluhu lakini imeshindikana kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine ya kikazi na hivyo Waziri Mwigulu atamwakilisha katika uzinduzi wa tamasha hilo.

 

Mbali na Mwigulu, viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, Angelina Mabula, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed  Msangi.

 

Aidha, Msama amesema kwamba katika tamasha hilo kunatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya waimbaji wa kitaifa na kimataifa na akawataja baadhi ya waimbaji ambao tayari wamethibitisha kuhudhuria kuwa ni, Rose Mhando, ambaye atazindua albamu yake mpya ya ‘Usivunjike Moyo’,  Angel Benard, Bonny Mwaitege, Jesca Honore, Christina Shusho, Christopher Muhangila, Upendo Nkone na wengine kibao.

 

“Niwaambie ndugu waandishi wa habari, maandalizi yanaenda vizuri kwani tumejipanga vyema kuhakikisha wananchi watakaofika siku hiyo wanapata burudani ya kutosha na kulishwa neno la Mungu kupitia ujumbe wa nyimbo za waimbaji na ulinzi wa kutosha utakuwepo kwani tayari jeshi la polisi litakuwepo kuhakikisha amani na utulivu upo na hivyo nawaomba wakazi wa maeneo hayo wajitokeze kwa wingi,” amesema.

 

Amebainisha kuwa viingilio siku hiyo kwa wakazi wa Mwanza na maeneo mengine yanayozunguka eneo hilo kwamba vitakuwa ni Shilingi 5,000 kwa wakubwa na  shilingi 2,000, kwa watoto huku kwa Mkoa wa Simiyu Aprili 2 mwaka huu, wakubwa  wataingia kwa shilingi 3,000 na watoto 2,000.