×

Okwi Ageuka Gumzo Uarabuni

MSHAMBULIAJI Emmanuel Okwi amekuwa gumzo kubwa hapa jijini Port Said kutokana na kiwango alichokionyesha katika mechi dhidi ya Al Masry ya hapa.

Okwi alionyesha kiwango kizuri wakati Simba ilipoivaa Al Masry katika mechi ya Kombe la Shirikisho iliyoisha kwa sare ya bila mabao.

 

Kiongozi mmoja wa Simba amesema Al Masry wameonyesha nia ya kumpata Okwi.

“Wameulizia kuhusiana na Okwi kama anaweza kupatikana na bei kiasi gani. Wameambiwa wafuate taratibu sahihi na majibu yote watayapata kwa utaratibu sahihi,” alisema.

 

Kama Simba itafanikiwa kumuuza Okwi, itakuwa ni mara ya pili kumuuza Uarabuni. Kabla iliwahi kumuuza katika kikosi cha Etoile Du Sahel ya Tunisia. Okwi, alionekana kupiga chenga nyingi nzuri na mashuti yaliyoleta hatari katika lango la Al Masry huku akipiga pia krosi makini.

 

Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Okwi aliwakimbiza pia Waarabu huku pia akifunga bao la kusawazisha kwa upande wa Simba ilipokuwa nyuma kwa mabao 1-2, na mwisho akaiwezesha timu yake kupata sare ya mabao 2-2.

Kwenye Ligi Kuu Bara, Mganda huyo anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 16 akifuatiwa na Obrey Chirwa wa Yanga mwenye mabao 12.

Saleh Ally, Port Said.