BAADA ya kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Klabu ya Township Rollers ya Botswana, Yanga imepata pigo zaidi baada ya beki wake wa kutumainiwa, Kelvin Yondani kutarajiwa kukaa nje kwenye Kombe la Shirikisho kutokana na kuwa na adhabu.
Yondani ambaye amekuwa msaada mkubwa kwenye beki ya Yanga, anatarajiwa kuukosa mchezo wa kwanza wa timu hiyo wa Kombe la Shirikisho baada ya kupata kadi za njano katika michezo miwili dhidi ya Waswana hao katika Uwanja wa Taifa jijini Dar na jijini Gaborone, Botswana.
Mlinzi huyo atakosa mechi hiyo ya Shirikisho Afrika ambapo Yanga itakutana na timu ambazo zimefuzu katika hatua ya kwanza ya kombe hilo kwa ajili ya kutafuta timu ambazo zitaenda makundi ya kombe hilo, ambapo Yanga watacheza mchezo wao wa kwanza katika Uwanja wa Taifa, Aprili 6, mwaka huu.
Yondani atakosa mchezo huo kutokana na kanuni za kadi ambazo zimewekwa na Shrikisho la Soka Afrika (Caf) ambapo mchezaji akiwa na kadi mbili atakosa mchezo unaofuata kwa ajili ya kufuta kadi hizo.
Kwenye hatua hiyo, Yanga iliyoondoshwa Ligi ya Mabingwa kwa mabao 2-1, ina uwezekano wa kukutana na timu za Enyimba ya Nigeria, CS La Mancha ya DR Congo, Supersport ya Afrika Kusini, Al Masry ya Misri, CR Belouizdad ya Algeria, Raja Casablanca ya Morocco, RS Berkane Morocco na El Hilal El Obayed ya Sudan.
Said Ally, Dar es Salaam.