×

KIFO CHA TAJIRI SUPER SAMI, MKE MDOGO AMFICHUA MUUAJI! – VIDEO

 

MAPYA yameibuka kufuatia kifo cha mfanyabiashara ambaye ni tajiri wa mabasi ya Kampuni ya Super Sami, Samson Josiah almaarufu Super Sami, mkazi wa Magu, Mwanza baada ya wake zake kufunguka na kueleza ya moyoni kuhusu tukio hilo la kusitisha huku mkewe mdogo akimfichua anayemhisi kuwa muuaji, Ijumaa Wikienda linaripoti.

 

Mfanyabiashara huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku kadhaa, kabla mwili wake kuonekana katika Mto Ndabaka wilayani Bunda mkoani Mara ukiwa umefungwa kwenye kiroba na kuharibika vibaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jafari Mohamed alieleza kuwa, hadi mwishoni mwa wiki iliyopita Jeshi la Polisi lilikuwa limewashikilia watu wanne kutokana na upelekezi uliofanyika. Alisema kuwa, mwili huo ulikutwa na baadhi ya wananchi waliokuwa mtoni hapo ambao walilazimika kutoka taarifa polisi.

 

KAULI ZA WAKE ZA MAREHEMU

Kwa nyakati tofauti wake wa marehemu walizungumza na Ijumaa Wikienda na kutoa maoni yao, huku wakieleza mambo wanayoamini kuwa yanaweza kuchangia kifo cha mume wao.

Mke mdogo.

 

MKE MDOGO

Naye Josephine ambaye ni mke wa pili wa marehemu, mbali na kueleza masikitiko yake kufuatia kifo hicho, alitumia muda mwingi kueleza jinsi mumuwe huyo alivyoondoka nyumbani hapo na kupotelea kusikukojulikana.

 

Alisema kuwa, siku ya tukio, mumewe aliondokea kwake kwenda safari zake za kawaida ingawa hakumweleza anakwenda wapi.

“Hakuondoka na chochote na sikuwa na wasiwasi kwa maana alikuwa anapatikana tu kwenye simu yake,” alisema na kuendelea:

Mwili wake ulivyookotwa.

 

“Lakini cha kushangaza siku hiyo hakurudi na kesho yake simu yake ikaanza kutopatikana. Nikaanza kuwaeleza wenzangu kuhusu jambo hilo. Lakini wao walishauri kuwa tusubiri huenda amesafiri nje ya nchi kama Kenya au Burundi na atarudi.”

 

Alisema kuwa, kadiri siku zilivyosonga, ndivyo alivyozidi kuwa na shaka kuhusu usalama wa mumewe huyo.

“Rafiki zake wakakusanyika nyumbani na kukubaliana kuanza kumtafuta kwa nguvu zote sasa. Wakaanza kutoa taarifa polisi na kwa ndugu wengine, lakini hakupatikana kokote,” alisema na kuendelea:

“Baadaye tukaja kusikia taarifa za kupatikana kwa gari lake kule Serengeti, lakini yeye akiwa hayumo na ndipo baadaye tena tukasikia kuwa mwili wake umeokotwa mtoni ukiwa umefungwa kwenye kiroba. Kwa kweli binadamu wabaya, inauma sana.”

Mke mkubwa.

MKE MKUBWA

Mke wa kwanza aliyejitambulisha kwa jina la Lilian Limbe alitumia muda mwingi kueleza masikitiko yake juu ya maisha baada ya kuondokewa na mumewe huyo, huku akiiomba serikali isaidie kupatikana kwa wauaji hao ili haki itendeke.

Alisema kuwa, kifo cha mumewe ni pigo kubwa kwake na familia kwa jumla na kimempa changamoto mpya juu ya namna ya kulea familia hiyo, hususan kuwasomesha watoto watatu alioachiwa na mumewe na kuwapatia matumizi mengine.

“Kifo cha mume wangu kimeniachia changamoto kubwa ya kulea watoto. Ninaiomba polisi isadie kupatikana wauaji hao ili haki itendeki na serikali kuona namna ya kunisaidia kulea watoto watatu nilioachiwa, hususan katika suala la malipo ya ada za shule na fedha za kujikimu,” alisema mjane huyo.

Samson Josiah enzi za uhai wake.

NINI KIMETOKEA?

Alipoulizwa anaweza kulihusisha tukio hilo na jambo gani, Josephine alisema kuwa anamhisi mtu mmoja aliwahi kufika nyumbani kwao na mkewe na kutambulishwa kwake na mumewe kama rafiki yake.

 

Alisema: “Mtu huyo amekuwa akija nyumbani mara kadhaa na kulala na mkewe. Siku moja wakati mume wangu akiwa hayupo, mtu huyo akaja na mkewe na kunieleza kuwa wametoka safarini Dar es Salaam, wakalala nyumbani na kuondoka siku iliyofuata.”

Alisema kuwa, mume wake aliporudi, alimweleza kuwa yule rafiki yake ambaye sasa alianza kufahamika pale nyumbani kama Anko, alifika na mkewe, wakalala. “Lakini mumewe wangu alionekana kutopenda jambo hilo,” alisema na kuongeza:

Jeneza likiwekwa kaburini.

 

“Alisema (mumewe) sitaki kusikia tena kwamba huyu jamaa anakuja hapa. Ni mtu ambaye simpendi kwa sababu aliwahi kuniuzia gari, nikamlipa fedha yake yote, lakini baadaye alinigeuka kuwa sijamlipa na suala hilo likafika hata polisi. “Kimsingi sitaki aje tena siyo mtu mzuri kwangu, namdai fedha zangu nyingi sana, lakini hataki kunilipa na kibaya zaidi ananifuatilia.”

Josephine alisema kuwa, tangu wakati huo hajamwona tena yule jamaa nyumbani hapo hadi mauti yalipomkuta mumewe.

“Nikiulizwa leo ninawaza nini kuhusu kifo hicho, ninachoweza kusema ni kwamba kwa mdomo wake, mume wangu aliwahi kunionya kuhusu rafiki yake huyo,” alisema mwanamama huyo akiangua kilio.

Waombolezaji wakiwa msibani.

 

POLISI WANASEMAJE?

Mfanyabiashara huyo alidaiwa kutoweka nyumbani kwake eneo la Mwananchi- Buzuruga, Kata ya Mahina, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza Februari 27, mwaka huu.

Wakati anaondoka nyumbani kwake alikuwa na gari lake aina ya Nissan Patrol lenye namna za usajili T 323 BSF.

 

Gari hilo lilipatikana Machi 9, mwaka huu likiwa limeteketea kwa moto katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Pembeni mwa gari hilo kulikuwa na panga na kiberiti ambavyo vilisemekana viliwekwa na waliohusika na uharifu huo.

Shughuli ya mazishi.

 

 

Awali, kamanda Mohamed alisema kuwa, baada ya polisi kubaini mwili huo na kwa kuwa kulikuwa na taarifa za ndugu wa jamaa huyo kumtafuta, jeshi hilo liliwasiliana nao kuja kumtambua na waliweza kumtambua kuwa ni ndugu yao.

 

Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na polisi katika upelelezi unaoendelea ili kuwabaini waliohusika na kifo hicho na kuwafikishwa kwenye vyombo vya dola ili haki ikatendeke.

Ili kuona video za mahojiano hayo na mazishi kwa jumla, tembelea Global TV Online kwenye Mtandao wa Youtube.

Stori: Mwandishi Wetu, Mwanza.

 

VIDEO: MSIKIE AKIFUNGUKA HAPA