
KUFUATIA kukithiri kwa matukio ya uhalifu kila siku, wananchi wenye hasira kali wamevamia kituo cha polisi kisha kukizingira, wakitaka kukichoma ili wamchomoe mtuhumiwa kwa lengo la kumuua, Ijumaa Wikienda lilifika kwenye eneo la tukio.
WIZI WA BODABODA
Tukio hilo lilijiri wiki iliyopita majira ya mchana kwenye kituo kidogo cha polisi cha Mji Mpya mjini hapa ambapo jamaa aliyetuhumiwa kukubuhu kwa wizi wa pikipiki almaarufu bodaboda alikuwa amehifadhiwa kituoni hapo.
Dakika chache baada ya mtuhumiwa huyo kuingia kwenye ‘rada’ za wananchi hao, Ijumaa Wikienda lilifika kituoni hapo na kushuhudia kundi kubwa la wananchi waliokuwa wamefunga mtaa, wakiwa na hasira kali ambao walikuwa wamekizingira kituo hicho wakishinikiza mtuhumiwa huyo atolewe nje ili wamalizane naye.

POLISI WATUMIA NGUVU
Kufuatia hali hiyo, polisi watatu wa kituo hicho walimfungia ndani mtuhumiwa huyo huku wakitumia nguvu kuwazua baadhi ya wananchi hao na kuwasiliana na wenzao wa kituo kikuu ili kupata msaada.
Muda mfupi baadaye, difenda lililojaa polisi waliovalia sare za polisi na za kirai wakiongozwa na Afande Clement Bazo, wakiwa na silaha za moto, walitinga kituoni hapo na kuwatawanya wananchi hao.
DAMU CHAPACHAPA
Baada ya zoezi la utawanyaji, polisi hao walimtoa mtuhumiwa huyo aliyekuwa ametapakaa damu chapachapa kutokana na kichapo cha awali kabla ya kuokolewa na polisi ambapo walinmchukua na kwenda ‘kumpumzisha’ kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro ‘Sentro’ kwa ajili ya kumuokoa na kifo kutoka kwa raia.
Wakizungumza na Ijumaa Wikienda, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, ldd Athuman na Kobelo Juma almaarufu KB ambao wote ni madereva wa bodoboda walikuwa na maoni tofautitofauti.

IDD ATHUMAN
“Huyu jamaa ni mtuhumiwa wa wizi wa bodaboda. Huwa anatumia ujanja wa hali ya juu na anadaiwa kutekeleza matukio ya wizi huo zaidi ya mara tatu. Hapa naona arobaini yake imefika.
”Ujanja anaotumia, huwa anakuja kijiweni anashinda kutwa nzima huku tukipiga naye stori bila kujua lengo lake. Anafanya hivyo kwa wiki moja hivi, akishazoeleka, anatafuta pikipiki mpya kijiweni, anaikodi aendeshe mwenyewe kwenye safari zake.
“Kwa kuwa anakuwa amezoeleka, anapatana bei na mhusika kisha anaondoka na bodaboda jumla.
“Inasemekana kwamba huwa anakwenda kuziuza huko wilayani Kilosa, Kilombero na Mvomero.
“Kwa jinsi alivyo mjanja, akishaiba Kijiwe cha Mji Mpya, anarudi hapa mjini baada ya mwezi, anafikia kijiwe kingine cha mbali, nako anatumia ujanja huohuo na kuiba bodaboda.
“Sasa aliyeibiwa bodaboda hapa kwenye kijiwe chetu cha Mji Mpya mwezi uliopita ndo’ amekutana naye, akamuuliza bodaboda yake iko wapi.
“Katika kujishtukia, huyu mtuhumiwa alianza kukimbia ndipo akamuitia mwizi…watu wakamkamata na kumshushia kichapo cha nguvu kabla ya kuokolewa na polisi,” alisimulia Idd Athuman.

KB
Kwa upande wake KB alikuwa na haya ya kusema: “lnauma sana, bodaboda aliyoiba huyu jamaa nasikia ni ya mama mmoja ambaye alikopa pesa akainunua kwa lengo la kumpatia kipato cha kulea familia na bado ilikuwa ni mpya. Baada ya kuiiba huyu jamaa alikwenda kuiuza huko Kilosa.
“Kama unavyoona, watu wana hasira ndiyo maana wamevamia kituo cha polisi wakitaka kuchoma moto ili wamtoe nje wamuue, watu wamechoka na ujambazi kama huu ambao umekithiri.”
SERIKALI YA MTAA
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Simu B kata ya Mji Mpya, Said Mkwinda aliyekuwepo eneo la tukio alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
KAMANDA MORO
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Ulrich Matei alithibitisha kuokolewa kwa kijana huyo ili ahukumiwe kwa sheria na kukemea tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
STORI: DUNSTAN SHEKIDELE, MORO.