
RAIS wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amekamatwa kwa madai ya kupokea Paundi milioni 42 (sawa na Sh. bilioni 132) kwa ajili ya kampeni, kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya, marehemu Muammar Gaddafi.

Sarkozy mwenye umri wa miaka 63 alikamatwa na polisi ambapo alihojiwa kutokana na fedha aliyoitumia katika kampeni ya uchaguzi ambayo aliipata mwaka 2007, kwa mujibu wa gazeti la Le Monde. Sarkozy anasemekana alipata fedha hiyo iliyomfanya akashinda uchaguzi na kushika madaraka kwa miaka mitano.

Sheria za Ufaransa zinakataza wagombea kupata fedha taslimu zaidi ya Paundi 6,300 ambazo ni sawa na Sh milioni 17,478,252. Fedha hizo zinasemekana zilipitia katika akaunti za benki zilizopo Panama na Switzerland kabla ya kumfikia Sarkozy.

Katika hali hiyo, Sarkozy analazimika kuelezea madai hayo ya wapinzani wake kuhusu alivyopata fedha hiyo katika muda wa saa 48 kabla hajafunguliwa mashtaka ya rushwa. Katika hati iliyopatikana hivi karibuni jijini Paris, inaonyesha kwamba kiongozi huyo wa Ufaransa na dikteta huyo wa zamani wa Libya walikubaliana kuhusu fedha hiyo kwa mujibu wa hati iliyoandikwa Kiarabu na kusainiwa na Mussa Kussa, aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi enzi za utawala wa Gaddafi mwaka 2006.
Hati hiyo inaelezea “makubaliano ya kumuunga mkono mgombea wa urais, Nicolas Sarkozy, kwa Euro milioni 50, ambazo ni sawa na Paundi milioni 42 au Sh. bilioni 132.