
BAADA ya kikosi cha Yanga hivi karibuni kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha mkuu wa timu hiyo, Mzambia, George Lwandamina, amesema kuwa hawatafanya makosa tena kwenye uwanja wa nyumbani katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Jumamosi iliyopita, Yanga iliiaga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutandikwa kwa jumla ya mabao 2-1 na Township Rollers ya Botswana katika mechi ilizokutana na timu hiyo.
Yanga ilifungwa mabao hayo katika mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Dar es Salaam na ile ya marudiano iliyofanyika Botswana matokeo yalikuwa ni 0-0.
Akizungumza na Championi Jumatano, Lwandamina amesema kuwa baada ya kutupwa nje katika michuano hiyo na kuangukia katika ile ya Kombe la Shirikisho Afrika, watahakikisha wanafanya vizuri katika mechi zote watakazocheza nyumbani.
Alisema kushindwa kwao kupata ushindi katika uwanja wa nyumbani, ndiyo kumesababisha waondolewe katika michuano hiyo hivyo hawataki tena jambo hilo litokee.
“Tumejifunza na sasa tunajipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi za nyumbani, kama tungefanya vizuri katika mchezo wetu wa kwanza tungesonga mbele.
“Vijana wangu walijitahidi sana kupambana katika mchezo wetu wa marudiano dhidi ya Township Rollers lakini tulishindwa kupata ushindi, kwa hiyo katika mechi zetu zijazo ni lazima tufanye vizuri nyumbani,” alisema Lwandamina.
Wakati Lwandamina akisema hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika ameliambia Championi Jumatano kuwa baada ya kuzikosa shilingi bilioni 1.3 ambazo wangezipata kama wangeingia kwenye hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa wanawinda milioni 600.
“Lengo letu lilikuwa ni kufika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini haikuwa hivyo na kujikuta tukiangukia katika hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho.
“Kwa hiyo, tunajipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika hatua hiyo ili tuweze kuingia hatua ya makundi ili tuzoe kitita cha fedha ambacho hutolewa, tutapambana haswa,” alisema Nyika.