
WAKATI wanariadha kutoka duniani wamekusanyika hapa Valencia, Hispania tayari kwa Mashindano Makubwa ya Dunia ya Riadha Nusu Marathon, Tanzania imekosa mwakilishi.
Tanzania kabla ilikuwa iwakilishwe na Wanariadha tisa, kabla baadaye kukutana na ‘zengwe’ la wanariadha hao ambao ni watumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kuitwa kambini kwa ajili ya kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi na baadaye kubaki wawili ambao wangewakilisha, nao wamegonga mwamba.
Taarifa za kugonga mwamba kwa hao wawili ambao ni Ezekiel Ngimba na Jacklin Sakilu ambao nao wote wanatoka katika timu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), zimetolewa hapa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Wilhelm Gidabuday, ambaye amesema wanariadha hao wamekosa ruhusa kazini kwao.
Hili ni pigo kubwa kwa mchezo huu ambao miaka ya nyuma ulituletea heshima kubwa kabisa, lakini sasa unaelekea kabisa kupotea na kuwaachia wenzetu wa Kenya watambe wanavyoweza na mchezo huu.
Gidabuday amelazimika kuja hapa Valencia akiwa mikono mitupu bila ya wanariadha na amekuja kuhudhuria mkutano tu huku nchi kadhaa duniani wakiwemo majirani zetu Kenya, Uganda, Ethiopia na Rwanda, wanariadha wake wapo hapa tayari kwa mashindano haya ya dunia ya Nusu Marathon.
Kuna mtu mmoja aliwahi kusema aliyeturoga katika michezo amekufa, inawezekana niliichukulia kauli hii kuwa ni utani lakini sasa naiona kama ina ukweli. Hivi kweli wanariadha wananyimwa ruhusa ya kuja hapa? Hapa walikuwa wanakuja kulipigania taifa na kama tungepata medali sifa ingeenda kwa taifa lakini leo hii tunabaki wasindikizaji.
Mashindano haya yangetumika pia kwa maandalizi kwa vijana wetu kabla ya kwenda Gold Coast, Australia mwezi ujao katika michezo ya Jumuiya ya Madola. Kweli bado tuna ndoto ya kuja kupata medali hapo mbele? Hakika tuna safari ndefu sana.
Wakati wenzetu wanatumia michezo kama kichocheo cha ajira siye tunaiona haina thamani kabisa, sijui lini tutaamka katika usingizi mzito tuliolala.
Kama tunashindwa kuleta timu katika mashindano makubwa kama haya hata wenzetu wanatuonaje?
Wanaikumbuka ile Tanzania ya zamani iliyokuwa na wanariadha wakaleta heshima duniani. Tanzania ya akina Filbert Bayi, Selemani Mujaya Nyambui na akina Gidamis Shahanga leo iko wapi?
Hawa walipambana na kuleta heshima na kujenga majina ambayo mpaka leo kwenye medani ya Riadha yanakumbukwa.
Kama tumeshindwa kuleta wanariadha hapa na wakapambane na kujiandaa vyema kwa michezo ya Jumuiya ya Madola mwezi ujao na Olimpiki mwaka 2020 Tokyo, Japan kuna haja ya kwenda pia huko? Hilo ndio swali nimekaa nawaza wakati mbele yangu nikiwaona wanariadha wa Kenya wakiwa wamewasili hapa na tambo kibao za kuchukua medali.
Ndoto za mwanariadha Alfonce Felix Simbu ambaye alikuwa anataka kutuletea medali nyingine kupitia mashindano haya na yale ya Japan ya Olimpiki zimeyayuka.
Simbu ni miongoni mwa wanariadha waliokuwa wanajianda na mbio hizi za Valencia kabla ya kuitwa kambini jeshini kwenda kwa mwajiri wake.
Hakika naandika haya huku huzuni kubwa ikinigubika, vile ninavyowaona wanariadha wengine hapa na bendera za nchi zao najiuliza tumekumbwa na nini Tanzania.