


WAFANYAKAZI wa Benki ya NMB Tanzania Kanda ya Mashariki wametoa msaada wa Shilingi Milioni 13 kwa Hospitali ya CCBRT ili kufanikisha upasuaji kwa akina mama saba wenye Fistula.
Akizungumza kuhusu msaada huo, Meneja wa kitengo cha Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) cha benki ya NMB, Lilian Kisamba, alisema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa wafanyakazi wa benki hiyo ambao wamejiwekea kusaida jamii yenye uhitaji wakisaidina na kitengo cha CSR.
Alisema kwa ujumla wa wafanyakazi wa benki hiyo wamekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii kupitia programu yao ya “staff initiative” ambao ni mpango ulio kwa kitengo cha uwajibikaji ili kusaida matatizo mbalimbali ambayo yanaikabili jamii.
Kutokana na hali hiyo wafanyakazi wa Kanda ya Mashariki wakisaidina na kitengo cha CSR wamefanikiwa kuchanga sh. Milioni 13 mbazo wamekabidhi uongozi wa Hospitali ya CCBRT ili kufanikisha upasuaji wa akina mama wenye fistula.
“Leo hii tumekabidhi mfano wa hundi ya Sh. 13 milioni ili kufanikisha upasuaji wa akina mama wenye fistula,” alisema Kisamba na kuongeza.
“Wafanyakazi wa NMB ndio wametoa pesa hizo kutoka mifukoni mwao lakini pia wanapata mchango kutoka kitengo cha uwajibikaji kuwaongezea pale walipotoa ili kufanikisha upasuaji kwa wanawake waliopo CCBRT.” alisema.