×

Polepole Aanika Utaratibu wa Kumpata Mgombea Ubunge CCM – Video

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa katibu wa Itikadi na uenezei wa Chama hicho, Humprey Polepole kimetoa utaratibu na ratiba kamili itakayoohusisha mchakato wa uchukuaji fomu kwa wagombea wa udiwani/masheha na wabunge/wawakilishi kupitia tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020.

 

“Fomu za udiwani ni Tsh 10,000, hii haizuii kamati za siasa za halmashauri husika kuweka michango japo si lazima, ni hiari, fomu za ubunge na uwakilishi ni Tsh 100,000, fomu za Uspika ni Tsh 500,000 na fomu za urais ni Tsh 1,000,000.

 

“Tarehe 14-17, Julai 2020, itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu ya ubunge wa jimbo, muda ni saa 2 hadi saa 10:00 jioni.

 

“Julai 14-17, ni kuchukua fomu za kugombea ubunge wa viti maalum, Julai 23 ni Mikutano Mikuu ya UWT ngazi ya Mkoa kupiga kura za maoni kwa wagombea wa viti maalum. Julai 30, kitaketi kikao cha Baraza la Vijana la mkoa kupiga kura za maoni viti maalum kundi la vijana.

“Kati ya Tarehe Julai 20-21, mikutano mikuu ya CCM ya Majimbo, au wilaya zitapiga kura za maoni kwa ubunge na wawakilishi. Julai 30, vikao vya kamati za siasa vya jimbo, kujadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa wagombea.

“Aug.1-2, vitaketi vikao vya kamati za siasa za wilaya kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mkoa. Aug.4-5, vitaketi vikao vya kamati za siasa za mkoa kujadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Kura za maoni Madiwani: “Tunaanza na Mkutano Mkuu wa Kata, mabalozi wa shina watashiriki, pale zitapigwa kura za maoni kwa wagombea wote, kisha vikao vya kuwachuja na kuweka mapendekezo vitaanza kuanzia Kata, Wilaya hadi Halmashauri Kuu ya Mkoa ambayo itatoa jina moja.

Uteuzi Wabunge: “Tutaanza na mkutano mkuu wa Jimbo, wagombea wote watajielezea, pale watapigiwa kura za maoni, kisha vitaanza vikao vya kamati za siasa kuwajadili na kuwaandikia watu watatu ‘wamependekeza’ sambamba na kura zao, kisha wilaya na baadaye mkoa.

“Baada ya Mkoa majina yatapelekwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kisha Kamati Kuu itapendekeza na mwisho Halmashauri Kuu ya Taifa ambao watajadili na kuteua jina moja ambalo ndiye atakuwa mgombea kwa tiketi ya CCM.”

“Ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mgombea kutoa au kupkea rushwa katika jitihada zake za kugombea kusaka uongozi. Wewe toa rushwa sisi tunafuatilia, tumejipanga TAKUKURU hawa ni watu wa kushughulika nao. Wabunge wa CCM leo mwisho, kesho sote tuko sawa.

“Mchakato wa kupiga kura za maoni CCM unatakiwa uwe wa wazi, wekeni masanduku ya kura mbele ya wajumbe wote na wagombea washiriki kuhesabu kura zao kila mmoja za kwake, tunataka uchaguzi uwe huru na wa haki. Kama mmejipanga vizuri wilayani mnaweza kurusha LIVE pia.

“Kwa niaba ya Uongozi wa CCM, ninawaonya muache mara moja kutumia mabango na vipeperushi mitandaoni kutia nia ya kugombea, ni kinyume na taratibu za chama chetu. ambao hawataacha tutaona namna ya kuwafanya,” amesema Polepole.

Leave a Comment