×

Mama Kanumba Atoswa Mazima!

WAMEMPOTEZEA? Ndivyo unavyoweza kujiuliza kufuatia mastaa wote wanaotamba mjini kushindwa kutokea kwenye hafla ya kumkumbuka ya miaka sita ya kifo cha aliyekuwa nguli wa sinema za Kibongo, Steven Kanumba (Kanumba Day) na kumwacha mama wa staa huyo, Flora Mtegoa aifanye shughuli hiyo akiwa na waigizaji wengi ambao hawana majina makubwa (maandagraundi).

 

Hata hivyo, kwenye shughuli hiyo iliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar, waigizaji pekee wakongwe waliojitokeza ni Emmanuel Myamba ‘Pastor Myamba’ na Stanley Msungu.

 

Mama Kanumba, akiwa na waigizaji hao wadogo makaburini hapo, walifanya maombi ya pamoja yaliyoongozwa na Pastor Myamba kama ishara ya kumkumbuka Kanumba aliyefariki Aprili 7, 2012.

Kama ilivyo desturi yake, mama Kanumba kila anapofanya kumbukumbu hiyo lazima aangue kilio, tofauti na siku nyingine ambazo hulia pamoja na baadhi ya mastaa wakubwa, siku hiyo alilia pamoja na maandagraundi.

Akizungumza mara baada ya ibada hiyo fupi, mama Kanumba alisema kuwa, anawashukuru wasanii waliojitokeza kwani wanaoneshwa ni jinsi gani wanaendelea kumuenzi Kanumba.

Alisema kuwa, kwa wale wasiofika, anawaombea Mungu awabadilishe na pia wajue kuwa kila nafsi itaonja mauti.

“Nawaombea wabadilike na watambue kwamba kila mtu atakufa hivyo ni vyema kukumbukana kama hivi inapotokea,” alisema mama Kanumba.

Kama hiyo haitoshi, katika mazungumzo yake na Ijumaa Wikienda, mama Kanumba pia hakusita kumtupia dongo mama wa muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’, Lucrecia Karugila ambaye bintiye ndiye alikutwa na hatia ya kumuua Kanumba bila kukusudia.

Alisema kuwa, mzazi mwenzake huyo anaonekana aliumia zaidi tu pale Lulu alivyohukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, kuliko kifo cha Kanumba.

“Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Mama Lulu yeye anaonekana aliumia zaidi wakati wa hukumu ya bintiye, kabla ya hapo sioni kama aliguswa na kifo cha mwanangu,” alisema mama Kanumba.

 

Kanumba alifariki Aprili 7, 2012 nyumbani kwake Sinza-Vatcan jijini Dar baada ya kutokea ugomvi kati yake na Lulu ambaye alikuwa mpenzi wake.

Lulu alidaiwa kumsukuma Kanumba, akaanguka na kupoteza maisha. Mrembo huyo yupo Gereza la Segerea akitumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia ya kuua bila kukusudia.

Stori: Gladness Mallya Dar.