
MKURUGENZI wa Kitengo cha Biashara cha Wateja wa Safaricom, Sylvia Mulinge, ameteuliwa kuwa mkuu wa kampuni ya Vodacom nchini Tanzania. Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bob Collymore, alitangaza uteuzi huo jana. “Mulinge ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji tangu Juni 1, 2018. Atachukua nafasi ya Ian Ferrao.
Katika utendaji kazi wake wa miaka 17, amejijengea sifa ya kuwa mmoja wa viongozi maarufu wa biashara. Ataacha timu yenye nguvu kubwa alikotoka,” alisema Collymore. Mulinge ana zaidi ya miaka kumi katika masuala ya masoko, ambako nusu ya miaka hiyo ameipitisha katika shughuli za mawasiliano.
Ana ujuzi mkubwa katika masuala ya masoko na uanzishaji wa brandi mbalimbali. Alijiunga na Safaricom mnamo Februari 2006 akitokea kampuni ya Unilever na kupanda kutoka Meneja wa Uzalishaji hadi Mkuu wa Mauzo ya Rejareja. Ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Nairobi (first class honours) katika Food Science and Technology.

Vilevile, alichaguliwa kwa kupigiwa kura na gazeti la Business Daily kuwa mmoja wa wanawake 40 mashuhuri zaidi nchini Kenya walio chini ya umri wa miaka 40.
Collymore alitangaza pia kwamba Charles Wanjohi atakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara ya Wateja ambapo atawajibika moja kwa moja kwake. Wanjohi, aliyejiunga na kamati ya utendaji ya Safaricom, ana miaka zaidi ya 15 katika shughuli za mawasiliano.
Alijiunga na Safaricom mnamo Juni 2015 kama Mkuu wa Vitengo vya Wateja na Masoko na alikuwa ndiye mwanzishaji wa kaulimbiu mbalimbali za biashara kama vile Stori Ibambe, Tunukiwa, Safaricom Platinum na BLAZE. Kabla ya kujiunga na Safaricom, alifanya kazi katika makampuni ya Eastman Kodak, Celtel Kenya, Zain na Airtel Group.