
Watawala wa Niger wamempa saa 72 Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo, wakiushutumu Umoja wa Mataifa kwa kuitenga Niger kwenye Mkutano mkuu mwezi uliopita.
Katika taarifa iliyosainiwa Oktoba 10, wizara ya mambo ya nje ya Niger imeamuru mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni raia wa Canada Louise Aubin kuondoka ndani ya saa 72. Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa mjini Niamey hajaeleza chochote.
Utawala huo wa kijeshi umeushutumu Umoja wa Mataifa kuwa walitumia kile walichokiita “ujanja usiofaa” uliochochewa na Ufaransa ili kuzuia ushiriki wake kamili katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa na mikutano mingine iliyofuata ya mashirika ya Umoja huo ambayo ilifanyika katika miji ya Vienna na Riyadh.
Maafisa wa jeshi walionyakua mamlaka katika mapinduzi mwezi Julai nchini Niger, hawakuwa na mwakilishi katika mkutano wa viongozi wa dunia huko New York.