×

Rihanna kwa Utajiri Alionao, Analala Saa 4 tu Usiku

Rihanna

KUNA muda unaweza kufika ukajiuliza mwanadada Rihanna, ambaye ni mwanamuziki maarufu duniani, kutokana na umaarufu wake, mafanikio ya kifedha na hadhi aliyonayo, anaendesha gari la aina gani, analala wapi, majirani zake nyumbani kwake ni kina nani, anapendelea vitu gani na mambo mengine mengi.

 

Kama umewahi kujiuliza au kuwaza maswali ya namna hiyo makala hii inakupa majibu. Sasa sikia;Kwanza, Rihanna ambaye ana asili kutoka Saint Michael visiwani Barbados, jina lake la kuzaliwa ni Rihanna Robin Fent na anamiliki utajiri unaokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 245, ambazo ni zaidi ya bilioni 500 za Kibongo.

 

Utajiri wake unatokana na kuuza muziki wake mitandaoni na albamu, matamasha, miradi anayomiliki na kutangaza pamoja na kuigiza, ambapo kutokana na vyanzo vyake vyote hivyo vya mapato Rihanna kwa mwaka jana tu anakadiriwa kukunja dola milioni 70, ambazo ni zaidi ya bilioni 140.

Fedha hizo alizipata kutokana na dili alilosaini la dola milioni 10 (bilioni 20) na Kampuni ya Louis Vuitton, kutangaza bidhaa zake za urembo. Lakini pia katika tamasha lake alilolifanya sehemu mbalimbali duniani lililokwenda kwa jina la Diamond lilimuingizia dola milioni 140 (zaidi ya bilioni 280).

Nyumba anazo miliki

Kwa Marekani, Rihanna anaishi katika mlima wa Beverly huko Los Angeles, Califonia. Katika mlima huo Rihanna anamiliki mjengo wenye vyumba vya kulala nane, mabafu 10, gym ya kufanyia mazoezi, bwawa la kuogelea na kilima kinachom-uwezesha kulitazama jiji hilo la Los Angeles, kwa utamu kabisa!

Gharama aliyotumia kununua mjengo huo inatajwa kufikia dola milioni 68, ambazo zinakimbilia milioni 300 za Kibongo. Katika makazi yake hayo watu maarufu ambao ni majirani zake ni Tom Cruise, Courtney Cox na muigizaji Jennifer Anniston. Lakini pia Rihanna ni anamiliki mjengo mwingine huko kwao Barbados, alioununua kwa dola milioni 22 (zaidi ya bilioni 44).

Magari

Rihanna anamiliki magari ya kifahari ambayo ni pamoja na Porsche 997 Turbo, Chevy Suburban, Lincoln Navigator, Maybach 57S na Lamborghini Aventador.

Mbwa

Rihanna anapenda sana mbwa na anamiliki mbwa aitwaye Panchito. Mbwa wake huyo amemtafutia rafiki zake ambao wanaishi pamoja ambao ni Oliver na Poodle.Anapendelea pia kuhusu kuvaa mavazi mazuri na ya bei mbaya pamoja na vito vya thamani.

Hivyo ni baadhi ya vitu ambavyo anamiliki Rihanna na amenunua kutokana na fedha zake. Lakini kuhusu utajiri wake huo, akizungumza na Jarida la Vougue Paris, Rihanna aliwahi kusema kwamba anajikuta akilala saa 4 tu kwa siku, na saa nyingine anafanya kazi ili kuhakikisha anautunza utajiri wake ili asije kurudi kwenye umasikini siku moja.