
KATIKA Tasnia ya Muziki anafahamika kwa jina la Jay Z, lakini mama yake mzazi Gloria Carter, alipomzaa alimuita Shawn Corey Carter, ambaye mbali na kujihusisha na Muziki wa Hip Hop, Jay Z ni mfanyabiashara, mume wa mwanamuziki wa R&B, Beyoncé Knowles, wana watoto watatu na wanaishi maisha ya kifahari usipime.
Kuiweka hii rahisi, Jay Z anakila kitu ambacho binadamu wa kawaida mwenye kupenda mafanikio anaota kumiliki. Kuanzia mke mzuri, watoto wazuri pamoja na mali nyingi ambapo kama huoni wivu twende kuzitazama.

Ghala ya magari
Jay Z kwenye suala la magari anakufuru usipime. Anamiliki magari tofautitofauti ambayo thamani yake inatajwa kufika dola za Marekani milioni 15, ambazo ni zaidi ya bilioni 33 za Kibongo.
Katika magari hayo kuna Pagani Zonda F, aliyoinunua zaidi ya milioni 134, Bugatti Veyron Grand Sport (bilioni 2), Bentley Azure (aliyozawadiwa na mkewe alipotimiza miaka 41), Maybach Exelero, Rolls Royce Phantom, Ferrari F430 Spider na Porsche 911 Carrera Cabriolet.

Nyumba
Baada ya kupata watoto mapacha mwaka jana, Jay Z na mkewe walinunua mjengo wa maana huko Los Angeles, wenye thamani ya bilioni 1. Mjengo huo una baa binafsi, sehemu ya kuogelea, vyumba vya kupokelea zawadi, vyumba vya midoli na vitu vingine mbalimbali.
Kabla ya mjengo huo wawili hao walikuwa pia wanamiliki mijengo sehemu mbalimbali duniani ikiwemo mijengo miwili iliyopo pale New Orleans’s Garden, New York na huko Florida.

Pete ya ndoa.
Mwaka 2008, Jay Z alimnunulia mkewe pete ya dhahabu ya Lorraine Schwartz kwa ajili ya ndoa yao. Pete hilo iligharibu takribani dola milioni 5 za Marekani (sawa na bilioni 11 za Kitanzania).

Ghala ya Saa na Cheni
Jamaa anapenda saa kinoma. Anamiliki saa za bei mbaya za dhahabu ikiwemo Hublot Big Bank, iliyogharimu bilioni 11 za Kitanzania, aliyozawadiwa na mkewe alipokuwa akitimiza miaka 43. Mbali na saa, Jay Z anapenda pia cheni za almasi na dhahabu. Cheni za mbei mbaya anazomiliki ni pamoja na Jesus Pieces, Roc-a-Fella Records, Layered, Dog Tag na cheni ya rozari ya dhahabu.
Ndege binafsi
Inaweza kukushangaza kidogo, lakini ukweli ni kwamba mkali huyu wa Hip Hop anamiliki ndege binafsi aina ya Bombardier Challenger 850, iliyogharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 40 ambazo ni bilioni 90 za Kitanzania.
Ndege hii Jay Z, alizawadiwa na mkewe katika Siku ya Kinababa Duniani, baada tu ya kumzaa binti yao, Blue Ivy.

Kisiwa
Jay Z anamiliki pia kisiwa huko Bahamas, ambacho alikinunua kwa fedha za Kitanzania zisizopungua bilioni 8.
Meli
Kwa kuwa anamiliki kisiwa na ndege ya kutua kisiwani hapo, pengine Jay Z aliona kwamba ni bora anunue meli ya kwenda kuegesha kisiwani hapo pia. Anamiliki meli aliyoinunua kutoka kwenye kampuni moja ya Nigeria iitwalo Kola Aluko, kwa zaidi ya bilioni 140 kwa ajili ya mkewe alipokuwa akitimiza miaka 32.
Meli hii kwa mwaka 2013, ndiyo ilikuwa inatajwa kuwa meli yenye kasi zaidi duniani na anaikodisha kwa milioni 18,000 za Kitanzania.
Farasi wa mashindano
Jay Z anamiliki pia farasi wa mashindano anayejulikana kwa jina la California Chrome aliyemnunua mwaka 2014, kwa zaidi ya bilioni 120 za Kitanzania kutoka kwa tajiri anayejulikana kwa jina la Kentucky.
BONIPHACE NGUMIJE