×

OPERESHENI YA MAKONDA ILIVYOLITIKISA DAR, WATU WAKESHA

NI wiki ya kitimtim! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutoa wito kwa wanawake waliotelekezewa watoto na wanaume kufika ofisini kwake, Ilala jijini Dar kwa ajili kupatiwa msaada wa kisheria.

 

Awali, zoezi hilo lililotarajiwa kudumu kwa takriban siku 5 mfululizo, lilianza kuchukua nafasi Jumatatu iliyopita ambapo mamia ya wanawake walijitokeza na kuifanya ofisi ya mkuu wa mkoa kufurika, hadi kufikia hatua ya kuzuia kwa muda safari za magari katika njia ambazo zinakutana katika ofisi hiyo.

Wanawake wasiopungua 480 walijitokeza ambapo kwa mujibu wa Makonda, 47 kati yao waliwataja waheshimiwa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku 14 wakiwa ni viongozi wa dini.

 

Akizungumza na wanahabari mara baada ya wanawake wengi kujitokeza na kusikilizwa na wanasheria mbalimbali pamoja na watu wa dawati la jinsia, Makonda alitoa wito kwa wanaume ambao wametajwa na wanawake wao waliowatelekeza, wajitokeze wenyewe ili kusikiliza kesi zao. Makonda alienda mbali zaidi kwa kuwataka wanaume ambao nao wametelekezewa watoto au wenye malalamiko mbalimbali dhidi ya wanawake, nao wafike ofisini kwake kwa ajili ya kusaidiwa.

 

WANAUME NAO WAJITOKEZA

Mara baada ya Makonda kutoa wito huo, Jumanne iliyopita wanaume walijitokeza katika ofisi yake na kutoa malalamiko mbalimbali.

Kuna ambao walidai kukimbiwa na wanawake wao kutokana na kuugua kwa muda mrefu, kuna wengine walilalamikia wake zao kugeuza nyumba kuwa danguro. Kama hiyo haitoshi, kuna mpiga picha maarufu wa Ilala jijini Dar, Vedasto Mdesa ambaye alisema amefika ofisini hapo ili kueleza jinsi alivyokimbiwa na mkewe.

 

“Mimi na mke wangu tulibahatika kuzaa watoto watatu, wawili wakiwa mapacha, mke wangu niliyezaa naye tulikutana hapa mjini akisoma Chuo Cha Kampala University na tulikuwa tunapendana lakini familia yake ndiyo haikukubali mimi kumuoa mwanamke huyo.

“Nimekuwa nikipata shida sana ya kukutana na mzazi mwenzangu kutokana na uchumi wangu kuwa mdogo kwani mimi ni mpigapicha tu eneo la Buguruni, nimekuwa nikipata vikwazo vingi kutokana na familia yangu kuwa ya kimaskini na mke wangu kutoka katika familia ya kitajiri, kiukweli mke wangu yeye anatoka familia ya kitajiri na ndugu zake wengine wanaishi Urusi na ndiyo hasa wanaosababisha mimi nisiishi na huyo mwanamke lakini bado nampenda na yeye ananipenda, cha msingi namuomba Makonda anisaidie niweze kurudishiwa familia yangu,” alisema paparazi huyo.

 

WATU WAKESHA

Kuonesha kwamba tatizo hilo ni kubwa, usiku wa kuamkia Jumatano, wapo akinamama ambao walidaiwa kukesha katika ofisi ya Makonda ili kuweza kuwahi foleni asubuhi na mapema.

 

BUNGENI KWATIKISIKA

Kuonesha kwamba jambo hilo ni nyeti, lililitikisa bunge ambapo wabunge mbalimbali waliotajwa na baadhi ya wanawake waliojitokeza kwa makonda, kuamua kujibu mashambulizi. Mmoja kati ya wabunge waliojitokeza hadharani na kujibu tuhuma za kudaiwa kutelekeza mtoto ni Mbunge Iringa Mjini, Peter Msigwa aliyesema kutajwa kwake katika operesheni ya Makonda ni mpango wa kumchafua.

Alisema: “Kuna propaganda za makusudi kujaribu kunichafua kuwa nimetelekeza mtoto Dar. Kama huyo mama ambaye jina lake limehifadhiwa yupo, nataka ajitokeze pamoja na mtoto niliyemtelekeza. “Kwa sasa nipo Dodoma Bungeni; anaweza kunipata kupitia Spika wa Bunge au Katibu wa Bunge au Kiongozi wa Upinzani Bungeni…Kama ikithibitika kuna mtoto nimemtelekeza nitajiuzulu ubunge.”

 

SPIKA AKIRI KITI KUTIKISIKA

Jambo hilo halikuishia kwa waheshimiwa wabunge tu, lilimgusa hadi Spika, Job Ndugai na kuamua kulizungumzia ambapo aliwataka wabunge washauri kitu cha kufanya ili kusaidia kutatua tatizo hilo.

“Kuna zoezi linaendelea huko Dar es Salaam sasa kidogo kiti cha Spika kimetikiswa hivi…tunatuhumiwa mahali kidogo, natarajia kupata ushauri wenu kama tunafanyaje katika hili maana kuna watoto wetu wapo barabarani na lazima tujue ni nini cha kufanya,” alisema Ndugai.

 

Spika Ndugai alienda mbele zaidi kwa kusema suala hilo si la wanaume tu kwani amepata taarifa kwamba wapo pia wabunge wanawake waliotajwa kuwatelekeza wanaume. Miongoni mwa matukio yaliyosisimua katika operesheni hiyo ya Makonda inayotarajiwa kufikia tamati leo, ni lile la mwanamke Safina Mohamed aliyezaa na raia wa China ambaye alifika kulalamikia ishu ya Mchina huyo kumtelekezea mtoto.

 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile naye alizungumzia suala hilo la Makonda kwa kusema ni lina tija lakini akashauri lifanyike kwa faragha kulingana na sheria inavyosema juu ya kuwaanika watoto wadogo. “Anachokifanya RC Makonda ni jambo zuri lakini linahitaji uangalifu na tufuate mifumo sahihi, nitoe rai kwa wananchi wote kufuata taasisi husika. Ushauri wangu kama Wizara inayosimamia Haki za Watoto, suala kama hili linatakiwa kufanyika faragha,” alisema Ndugulile.

MAKALA: Mwandishi wetu