×

Tambwe Aifungia Kazi Simba, Ajiongezea Programu

Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe (kushoto) akifanya mazoezi na Kamusoko.

KATIKA kuhakikisha anakuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa watani wa jadi Simba, mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, anajifua kikamilifu kuelekea mchezo huo huku akijiongezea programu maalumu ya mazoezi ya binafsi.

 

Tambwe alijiunga na kambi ya Yanga iliyoweka huko mkoani Morogoro tangu Jumatatu ya wiki hii akiwa na wenzake Kelvin Yondani, Hassan Kessy, Thabani Kamusoko, Ibrahim Ajibu na Andrew Vincent ‘Dante’ waliobakishwa Dar wakati timu hiyo ilipokwenda kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara na Mbeya City kutokana na majeraha pamoja na kadi tatu za njano.

 

Tambwe ambaye ni raia wa Burundi, hivi karibuni alirejea uwanjani na kuanza mazoezi mepesi ya binafsi kabla ya kujiunga na wenzake huko Morogoro baada ya kupona majeraha yake ya goti yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.

 

Daktari Mkuu wa Yanga, Edward Bavu, ameliambia gazeti hili kuwa Tambwe amekuwa akifanya mazoezi kikamilifu ya nguvu ya pamoja na wenzake katika kujiweka fiti.

 

Bavu alisema, tofauti na mazoezi hayo ya pamoja na wenzake, pia anafanya mazoezi mengine ya ziada ya binafsi ili kuhakikisha anapata ‘match fitness’ haraka kwa kuwahi mazoezi pekee na kukimbia mbio fupi na ndefu.

 

“Hatma ya Tambwe ya kucheza au kutokucheza ipo chini ya benchi la ufundi ambalo litaamua acheze au asicheze, lakini mimi kwa upande wangu niseme Tambwe yupo fiti,” alisema Bavu.

Stori: Musa Mateja na Wilbert Molandi