
YANGA kesho Jumapili inacheza mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini nchini Algeria dhidi ya Klabu ya USM Alger.
Ikiwa imeondoka jijini Dar es Salaam juzi Alhamisi, Yanga inacheza mechi hii bila ya nyota wake saba walioshindwa kusafiri na timu hiyo kwa sababu mbalimbali.
Hata hivyo, wachezaji hao ambao wengi walidai ni majeruhi hasa wakiwa wameumia katika mchezo dhidi ya Simba uliochezwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Habari za ndani ya Yanga, zinadai kuwa wachezaji hao wanadai mishahara yao ya nyuma na wamegoma kusafiri na timu hiyo kwenda Algeria wakishinikiza kulipwa mishahara yao.
Yanga inaonekana haina fedha kwa sasa lakini imekuwa ikiwaridhisha nyota wake kwa kuwapa ahadi ambazo hazitekelezeki hivyo sasa wachezaji hao wameamua kuwa ‘siriazi’ ili walipwe.
Mazingira ya Yanga kwa sasa yapo katika ngazi ya taifa, hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipaswa kufikiria zaidi na kusaidia kutatua tatizo hilo kwa maslahi ya taifa.
Ingetumika njia nyingine yoyote ile ili Yanga iweze kupata kiasi kidogo cha fedha ili kupunguza madeni ya wachezaji hao halafu baadaye klabu hiyo ingeweza kurudisha fedha hizo kuliko kuingia kwenye aibu iliyopo.
Hatuombei mabaya, lakini kesho Yanga ikipoteza mchezo kwa kufungwa mabao mengi na USM Alger lawama na aibu haitabaki kwa wachezaji peke yao bali raia wote wa Tanzania.
Yanga ni wawakilishi wa nchi, hivyo kuna wakati utaifa ungefaa kutangulizwa lakini na viongozi wake nao hawatakiwi kuona aibu kama hawana fedha, waombe ili wapewe.
Bodi ya Uhariri/Maoni | Championi Jumamosi