
BEKI Mghana wa Simba, Asante Kwasi amefunguka kuwa, haikuwa kazi rahisi kwao kufikia hapo walipo mpaka sasa wanaona wanaelekea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kwasi amesema ushirikiano wao ndiyo umewafanya kuwa hapo licha ya kwamba walikumbana na changamoto nyingi.
Mghana huyo ambaye kwa sasa ana mabao nane akiwa ndiye beki mwenye mabao mengi kwenye ligi hiyo msimu huu, amejiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo akitokea Lipuli FC.
Akizungumza na Championi Juma tano, Kwasi alisema kuwa ni vizuri na ni furaha kuona timu yake inafanya vyema na kuweza kufikia hatua ya kuelekea ubingwa jambo ambalo si rahisi.
“Nashukuru Mungu tunapambana na malengo yetu yanaenda kutimia kwa kiasi kikubwa, ni furaha kuweza kuona timu yako inatwaa ubingwa na kuweza kupata nafasi nzuri ya kujitangaza kimataifa, siyo kazi rahisi.
“Lakini ushirikiano wetu ndiyo umekuwa chachu ya mafanikio na kuweza kufika hapa tulipo siyo kazi rahisi changamoto ni nyingi lakini inabidi kupambana tu hakuna namna ili kuweza kutimiza malengo ambayo tumejiwekea mpaka sasa,” alisema Kwasi.
Stori: Martha Mboma, Dar es Salaam