×

Yanga Jifunzeni Kupokea Hata Vidogo

KW A N Z A kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza timu ya Simba kwa kuwa karibu kabisa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

Inahitaji pointi mbili tu ili iweze kutangaza ubingwa huo ambao kwa zaidi ya misimu minne ilikuwa ikipambana kuupata bila ya mafanikio.

 

Pongeza kwa wachezaji, viongozi wa benchi la ufundi pamoja na viongozi wote wa klabu hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya msimu huu na kuweza kufika hapo walipofika hivi sasa.

 

Uwekezaji mzuri walioufanya msimu huu ndiyo siri kubwa ya mafanikio hayo kuanzia katika usajili lakini pia kuimarisha uchumi wao kutokana na udhamini mbalimbali walioupata kutoka kwa SportPesa pamoja na Azam TV.

 

 

Lakini pia ushirikiano mzuri walionao kutoka kwa baadhi ya wadau wa soka nao pia umewezesha kuwa hapo walipo hivi sasa.

 

Baada ya kusema hayo machache nichukue nafasi hii kuizungumzia timu ya Yanga, timu yangu ya zamani ambayo nilichezea kwa mafanikio makubwa na kuniwezesha kuandika rekodi ya pekee ambayo mpaka sasa hajavunjwa.

 

Nikiwa Yanga nilifanikiwa kufunga mabao 26 katika msimu mmoja wa ligi kuu na kuweza kuibuka mfungaji bora wa ligi hiyo.

 

Hivi sasa hali ya kiuchumi katika Klabu ya Yanga siyo nzuri kabisa ukilinganisha na misimu mingine iliyopita wakati alipokuwepo Yusuf Manji ambaye alikuwa akiisaidia sana timu hiyo.

Hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wakigoma kwenda Algeria na timu hiyo kwa kile kinachodaiwa ni kutokana na kutolipwa mishahara yao kwa miezi mitatu.

 

Jambo hilo limesababisha Yanga ishindwe kufanya vizuri katika mechi yake dhidi ya USM Alger ya Algeria ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Kutokana na hali hiyo nichukue nafasi hii kuutaka uongozi wa Yanga kuanzia sasa ulichukulie saula hilo kama changamoto na kuanza kuandaa mikakati ya kuhakikisha unalimaliza.

Unatakiwa kulichukulia kwa ukubwa wa hali ya juu na uzito wa aina yake kama kweli unataka mafanikio ya klabu hiyo.

 

Kupitia kitengo chake cha masoko ambacho naamini kipo klabuni hapo, basi wahusika wanaohusika na kitengo hicho huu ndiyo wakati wa kuhakikisha wanaingia barabarani kwa ajili ya kutafuta wawekezaji.

Kwa ukubwa wa klabu hiyo na jina la klabu hiyo kama watu hao wa masoko watajipanga vizuri ni matumaini yangu watapata udhamini.

 

Wasiangalie ukubwa wa udhamini wanaoupata ila wanachotakiwa ni kuangalia utawasaidia kwa kiasi gani katika kukabiliana na hali ya sasa inayowaandama.

Kuna taarifa nilizipata kuwa mwanzoni mwa msimu huu Benki ya NMB ilitaka kudhamini klabu hiyo lakini uongozi wa Yanga walipoambiwa wapeleke bajeti yao, walipeleka ambayo iliwaogopesha NMB.

 

Lakini walipoambiwa wapunguze bajeti yao na kufikia kiasi ambacho kingewafanya NMB kudhamini klabu hiyo, viongozi hao walikataa.

Hali hiyo iliwafanya NMB waamue kuachana na klabu hiyo na kuendelea kujikita katika Klabu ya Azam ambayo yenyewe ilikubaliana na kiasi hicho cha fedha ambacho Yanga walikikataa.

 

Kutokana na hali hiyo, kama Yanga wangekubali kupokea kiasi hicho cha fedha wakajumlisha na kile cha SportPesa hakika ukata huu ambao unawakumba sasa usingekuwepo na kama ungekuwepo usingekuwa mkubwa kwa kiasi hiki.

Nimalizie tu kwa kuwaambia viongozi wa Yanga wajifunze sasa kutokana na kosa hilo walilolifanya, wasiwe wepesi wa kukataa udhamini, hata wakiwa na wadhamini 50 wa fedha kiduchu wachukue, utawasaidia katika kupunguza baadhi ya gharama za uendeshaji wa klabu.