
UNAPOZU-NGUMZIA wanamuziki wenye elimu ya juu Bongo, huwezi kuacha kulitaja jina la mwanamuziki, Nickson Simon ‘Nikki wa Pili’, ambaye ni miongoni mwa wakali wanaounda Kundi la Weusi, akiwa pamoja na kaka yake John Simon ‘Joh Makini’ na George Mdemu ‘G Nako’.
Nikki kichwani amemeza ‘masters’ katika masuala ya maendeleo (development studies) na ameweka wazi kwamba mara kwa mara amekuwa akikutana na maswali kutoka kwa watu kwa nini haajiriwi pamoja na kuwa na elimu ya juu kiasi hicho.
Sasa jibu la swali hilo, anatumiaje elimu yake katika maisha yake ya kawaida, ana mchumba na mipango ya kuoa, ana mtoto na mengine mengi kuhusu muziki na maisha yake ya kawaida, ungana naye kwenye mahojiano na Showbiz Xtra.
Showbiz Xtra: Nikki kwanza hongera, unafanya muziki mzuri na una watu wanaokufuatilia na kutamani kusikia mengi kutoka kwako.
Nikki: Asante sana.
Showbiz Xtra: Lakini mbali na muziki umekwenda shule na bila shaka una ‘PHD’ eeeh kwenye masuala ya maendeleo?
Nikki: Hapana ni masters.
Showbiz Xtra: Kuna kipindi ulisema unaendelea na PHD?
Nikki: Sikuendelea lakini baadaye nitafanya hivyo.
Showbiz Xtra: Sawa. Ushawahi kuimba wimbo kwamba hutaki kazi, lakini pengine kuna jibu tofauti na hilo kwa sasa, kwamba unaweza kuweka muziki kando na kuajiriwa?
Nikki: Hapana, muziki ni ajira yangu sina haja ya kuacha na kutafuta ajira nyingine. Unajua tunakwenda shule si tuajiriwe, tunakwenda shule kupata elimu na tuweze kujisaidia kwenye maisha yetu ya kawaida.
Showbiz Xtra: Sasa wewe kwenye muziki wako elimu inakusaidia nini, ukizingatia umesomea masuala ya maendeleo?
Nikki: Elimu ni pana sana. Haijalishi darasani unakuwa umesomea nini lakini ile elimu uliyonayo inaweza kukusaidia kwenye mambo mengine mengi. Mimi elimu yangu kwenye muziki inanisaidia kwenye mikataba, kujua huu mkataba una manufaa na mimi au la! Kuandika projekti, namna ya kujiendeleza zaidi kupitia kazi yangu kwa
maana nimesoma masuala ya kimae-ndeleo na mambo mengine. Lakini zaidi ninasaidia wengine kufahamu umuhimu wa elimu.
Show-biz Xtra: Unasaidia wengine kivipi?
Nikki: Kwa mfano kwa sasa ninaprojekti ya kuhamasisha watu kusoma vitabu. Maana kwenye vitabu ndiyo kuna maarifa mengi lakini vijana wa Kitanzania ni wavivu kusoma vitabu. Hapa nimeungana mkono na mwanamuziki anaitwa Siza, na tuna channel yetu kwenye mtandao wa YouTube, ambapo kuna vitabu mbalimbali tumeweka kwa ajili ya watu tusome.
Lakini pia tunatoa vitabu bure kwa watu ambao wameungana na sisi kwenye chaneli yetu hiyo YouTube, ni bure, wanasoma na kurudisha.
Showbiz Xtra: Hongera sana kwa hilo. Lakini pia ningependa kupata mtazamo wako kama Mwafrika na msomi, nini mtazamo wako kwenye kauli aliyoitoa hivi karibuni rapa Kanye West kwamba Waafrika walipenda kuwa watumwa?
Nikki: Ni kauli ya kipuuzi. Atakuwa hafahamu historia ya utumwa. Angekuwa anaifahamu historia asingeweza kuzungumza jambo la kipuuzi kiasi hicho.
Showbiz Xtra:Tukizungumzia Weusi, kuna kazi yoyote ambayo mnajipanga kutoa hivi karibuni?
Nikki: Ndiyo. Kuna kazi mbili ambazo tunatarajia kuzitoa mashabiki wetu wakae mkao wa kula. Lakini mimi pia kuna kazi nitaitoa hivi karibuni. Nipo peke yangu kwa hiyo tunakwenda kulisimamisha jiji hili soon?
Showbiz Xtra: Sawa. Weusi ni kundi, lakini ni kampuni vilevile. Ni hatua gani ambazo kama kampuni mmepiga na vyanzo vyenu vya pesa zaidi ni vipi?
Nikki: Kama kampuni tumepiga hatua kubwa sana na ndiyo maana bado tumesimama na tunajiendesha. Sisi si watu wa kuzungumza sana ‘material’ bali kuwapa mashabiki wetu kazi nzuri Kuhusu vyanzo vyetu vya pesa tunauza mavazi, nyimbo mtandaoni, tuna-piga shoo, madili kwenye makampuni mbalimbali na mambo mengine mengi.
Showbiz Xtra: Kwa mafanikio uliyonayo ni sahihi kukuita tajiri na kama ni tajiri, utajiri wako ni kiasi gani?
Nikki: Sitapenda kuzungumzia zaidi hili suala, kama nilivyosema awali mimi siyo mtu wa ‘material’ sana, kutaja nina nini na natarajia kufanya nini kwenye masuala yangu binafsi.
Showbiz Xtra: Una mchumba?
Nikki: Ndiyo.
Showbiz Xtra: Unaweza kumuweka wazi watu wakamfahamu.
Nikki: Hapana, hajatoa ridhaa yake.
Showbiz Xtra: Vipi kuhusu mipango yenu ya kufunga ndoa?
Nikki: Bado. Muda ukifika tutaweka wazi.
Showbiz Xtra: Una mtoto?
Nikki: Hapana.
Showbiz Xtra: Asante sana Nikki kwa ‘time’ yako. Lolote la mwisho kwa mashabiki wako.
Nikki: Tuendelee kupeana sapoti na kikubwa ninawapenda sana.
BONIPHACE NGUMIJE