
BODI ya Ligi Tanzania (TPLB) imethibitisha kwamba Simba hawatakabidhiwa kombe lao leo Jumamosi lakini litakuwa jipya na ghali kuliko yale yaliyopita.
Simba ambayo imetawazwa mabingwa wapya tangu juzi Alhamisi, Yanga ilipopigwa mabao 2-0 na Prisons mjini Mbeya, leo itacheza na Singida United ugenini katika mchezo ambao Msimbazi walitaka kupewa ‘ndoo’ yao kabisa waiwahishe Bungeni jijini Dodoma Jumatatu.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura aliliambia Championi Jumamosi kuwa, kombe la Simba litakuwa jipya kwa sababu lile la awali, Yanga wamelichukua moja kwa moja ni sawa na kusema watapewa kombe moto.
“Kutokana na Yanga kuchukua ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo, kombe watakalopewa Simba litakuwa jipya,” alisema kiongozi huyo ambaye pia kitaaluma ni mwanahabari.
Habari za ndani ambazo Championi imezipata ni kwamba kombe hilo bado halijatengenezwa ndiyo maana Simba hawawezi kukabidhiwa kwenye mchezo wa leo.

Habari zinasema kwamba vigogo wa Bodi ya Ligi wanakutana na wadhamini Jumatatu jijini Dar kujadili kuhusiana na muundo, aina na gharama za kombe hilo ambalo mashabiki wa Simba wanalisubiri kwa ‘mzuka’ mkubwa baada ya kulikosa kwa misimu mitano.
Lakini chanzo chetu kimetuthibitishia kwamba kombe la safari hii litakuwa ghali kuliko yale ambayo yamekuwa yakichukuliwa na Yanga misimu iliyopita na kwamba litakuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 10 na litatengenezwa Dar.
Alisema kwamba, wanataka liwe la gharama kubwa kutokana na thamani ya ligi hiyo kupanda pamoja na uwekezaji ulivyo.
TFF imepanga kuiandalia Simba sherehe kubwa ya kuwakabidhi ubingwa wao katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Jumapili ya Mei 20, kwenye Uwanja wa Taifa ikiwa ni siku mbili kabla ya mchezo wa Yanga na Mbao.
Simba imeweka rekodi ya kutofungwa mpaka sasa katika mchezo wa 27 huku ofisa habari wake, Haji Manara, akiomba wapewe ‘ndoo’ yao leo.
Juzi baada ya Yanga kupokea kichapo, Manara alisema: “Tunawaomba TFF, Bodi ya Ligi kwa ombi maalum watuletee uchampioni Singida, tumependa kombe letu tukabidhiwe huku kwa sababu tunataka kuwapa fursa wananchi wa mikoani na mikoa ya jirani wafurahie kombe na sisi mpaka tutakaporejea Dar.”
“Kuhusu shamrashamra za kurudi Dar na mapokezi tutawatangazia baadaye, kwa sasa tumepokea rasmi mwaliko wa kutembelea ofisi za bunge siku ya Jumatatu saa 4:00 asubuhi pale Dodoma.”
Wambura, alisema: “Kombe watapewa kwenye mechi yao dhidi ya Kagera, kwa sababu kupewa kombe kuna shughuli mbalimbali zinafanywa, sio kombe linatolewa tu na kukabidhiwa, bali kuna vitu vingi vinaandamana na hiyo shughuli.
“Kumbuka haya matokeo ya ubingwa yamepatikana jana (juzi Alhamisi), sasa hizo shughuli mpaka uzikamilishe zote ili kuifanya hiyo shughuli ya kombe Jumamosi haitawezekana.
“Na sisi wala hawakutuandikia kwamba wanataka wakabidhiwe kombe na ni wajibu wetu kuwapa kombe baada ya msimamo kutuelekeza kwamba wanastahili kombe.”
Baada ya mchezo wa leo, Simba itasaliwa na michezo miwili dhidi Kagera utakaochezwa Dar es Salaam na itamalizia msimu mjini Songea kwa kucheza na Majimaji ambayo inang’ang’ania kubaki ligi kuu.
Stori: Omary Mdose na Ibrahim Mressy