
CRISTIANO Ronaldo amesisitiza kuwa hafanani kwa chochote na Mohamed Salah wakati wakali hao wawili wakitarajiwa kuonyeshana umwamba kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumamosi.
Ronaldo ataiongoza Real Madrid wakati Salah akiiongoza Liverpool katika fainali hiyo ya kukata na shoka inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa NSC Olimpiyskiy jijini Kiev, Ukraine.

Ronaldo na Salah wote wamekuwa katika viwango bora msimu huu huku Ronaldo akiifungia Real Madrid mabao 43 na Salah akipiga 44 kwa Liverpool.
Ingawa wote Ronaldo na Salah wanatajwa sana kuwa watashindana kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia (Ballon d’Or 2018), Ronaldo amesisitiza hakuna ulinganisho wowote ambao unaweza kufanywa kati yao.
Akizungumza na BT Sport, Ronaldo amesema: “Watu wanataka kunifa-nani-sha mimi na wach-ezaji wengine, nipo tofauti na kila mmoja. Salah naye ni tofauti na wengine. Kwa hiyo tuko tofauti.
“Anacheza kwa kushoto, nacheza kwa kulia, mimi ni mrefu, yeye kidogo ni mfupi. Nacheza kwa kichwa changu, mnajua tuko tofauti sana. Lakini niseme tu kwamba amekuwa na msimu mzuri, lakini kwa Jumamosi (leo), ngoja tuone.”
Salah atakuwa akitafuta kushinda taji lake la kwanza kubwa la Ulaya, wakati Ronaldo atakuwa akijaribu kubeba ubingwa huo kwa mara ya tano hatua ambayo itamfanya awe mchezaji aliyefanikiwa zaidi katika historia ya michuano hiyo.