×

BAO LA ‘BAISKELI’ LA BALE LAZUA HEKAHEKA BONGO

Gareth Bale airuka hewani na kuunasa mpira.

BAO la ‘baiskeli’  (tiktak) alilofunga Gareth Bale dakika ya 64 kipindi cha pili jana, miongoni mwa mabao mawili aliyofunga na kumwacha kipa wa Liverpool, Loris Karius akiwa haamini kilichotokea,  lilizua hekaheka miongoni mwa wapenzi wa soka, wengi wao wakidai kwamba lilikuwa ni moja ya mabao mazuri zaidi ya michuano hiyo ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

…Akujiweka sawa kuruka zaidi.

Hekaheka za bao hilo zilijionyesha wazi katika vituo vya madereva wa Bajaj, bodaboda, katika mabaa na kadhalika ambako kulikuwa na ubishi wa kila aina ambapo mashabiki wa Liverpool leo hawakufika kwa ingi katika vituo vyao vya kazi kwa kukwepa maumivu ya kuzodolewa na wapenzi wa klabu ya Madrid.

…Tayari amepiga shuti.

Real Madrid jana iliandika historia ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ‘Uefa’ kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuilaza Liverpool mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa usiku wa kuamkia leo Jumapili kwenye Uwanja wa Olimpiyskiy mjini Kiev, Ukraine.

Bale alianzia kwenye benchi lakini kuingia kwake kuliiongezea nguvu Real Madrid kwani alipachika mabao mawili yaliyozima ndoto za Liverpool.

Kati ya mabao hayo, moja lilikuwa maridadi na litabakia katika historia ya mashindano hayo wakati jingine lilitokana na makosa ya kipa wa Liverpool, Loris Karius, ambaye alifungisha mabao mawili.

Mpira ukielekea golini.
Kipa Karius akiwa ndani ya goli lake baada ya mpira wa Bale kutinga wavuni.