
KUFUATIA kifo cha Mkali wa Bongo Fleva, Sam wa Ukweli ambaye leo anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Global TV Online imefika nyumbani kwao na marehemu kuhudhuria mazishi hayo ambapo imeelezwa namna ambavyo Sam wa Ukweli alidunduliza kidogo kidogo hadi akamjengea nyumba bibi yake aliyemlea.

Imeelezwa kwamba katika hustle za muziki, Sam alikuwa akimkumbuka sana bibi yake huyo, hivyo aliamua kuweka alama na shukrani kwa bibi yake huyo mlezi ili apate pa kujihifadhi kulingana na hali ya maisha ya kijijini licha ya kwamba nyumba hiyo ilikuwa kwenye hatua za mwisho kabla ya kifo chake.

Mbali na hilo, nyumba nyingine ya tope na nyasi iliyopo pale ni ile ambayo ndimo Sam wa Ukweli alizaliwa na kulelewa, ameiacha kama kumbukumbu kabla ya kujenga hiyo mpya.

Aidha, wasanii mbalimbali wamefika nyumbani kwao na Sam ili kujumuika na ndugu, jamaa na marafiki katika kumsindikiza marehemu kwenye safari yake ya mwisho hapa duniani aliyoikamilisha usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Palestina jijini Dar es Salaam alipoaga dunia.

Baadhi ya wasanii wa Bongo waliofika msibani hapo mpaka sasa ni Rapa Fid Q, Roma, Snura Mushi, Ben Pol, G Nako na wengine.

Pia viongozi wa vyama wa Serikali akiwemo Mbunge wa Chalinze, Bagamoyo, Ridhiwani Kikwete nao wamefika kuungana na waombolezaji katika maziko hayo.

Mwili wa Sam wa ukweli umeagwa leo asubuhi katika Hospitali ya Mwanyamala jijini Dar es Salaam na kusafirishwa kupelekwa kijijini kwao Kiwangwa kwa ajili ya mazishi.