
BOB Manecky ni mmoja kati ya maprodyuza naweza sema waliofanikisha kwa kiasi kikubwa safari ya muziki wa Juma Khalid ‘Jux’.
Nilianza kumjua Jux miaka nane iliyopita, enzi hizo akijiita Jux Vuitton ambapo alikuwa akipenda kupiga picha na nguo au bidhaa za Louis Vuitton kuanzia viatu mpaka kofia.
Ukiachilia hivyo, Jux alikuwa na uwezo mkubwa wa kuimba, anajua kupangilia mashairi, nilishawahi kumshuhudia akiingiza ‘vocal’ ndani ya Studio ya AM Records pale Tandale-Tanesco jijini Dar.
Nimpongeze ameweza kuuteka Muziki wa R&B Bongo na kuwa miongoni mwa wakali wanaokimbiza katika muziki huo akiwemo pia na Benard Paul ‘Ben Pol’.
Napata Raha ndiyo kibao kilichomuweka kwenye ramani ya muziki mwaka 2011 kisha zikafuatia ngoma kibao kama vile Uzuri Wako iliotoka mwishoni mwa 2012, Nitasubiri, Sisikii, Umenikamata na nyingine kibao.

Huyu ndiyo Jux bwana! Mbali na muziki, katika maisha ya kawaida, staa huyu ana uhusiano wa karibu na mwanadada Vanessa Mdee ‘Vee Money’, wawili hawa wanadaiwa kuwa ni wapenzi wanaoendesha uhusiano wao ‘kiintaneshino’.
Wakiwa pamoja, tayari wamefanikiwa kutoa ngoma za pamoja kama vile Juu, Mahabuba na Nimezama na zote zimebamba kinoma.
Jux kama Jux muziki wake haujaenda mbali sana kama ilivyo kwa mwenzi wake huyo ambaye nchi kibao za Afrika zinamtambua na kumkubali kama mpambanaji. Muziki wa Jux unaweza kusema umeishia Afrika Mashariki nikiwa na maana Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda.
Kilichonisukuma hadi kuandika makala haya ni juu ya muziki wa mkali huyu wa sauti kutokufika mbali na pia kutotumia fursa kwa mwenzi wake ambaye ameshajitanua katika soko la kimataifa.
Ukisikiliza kwa sikio la tatu, ngoma za Jux alizozitoa hivi karibuni kama vile Utaniua na Fimbo nadhani utanielewa namaanisha Jux ni wa kiwango cha aina gani katika Muziki wa R&B Bongo.
Zipo sababu unaweza kuona huenda zinachangia, asiweze kuliteka soko la kimataifa;

NI KUZUBAA
Inawezekana ikawa ni ‘point’ mojawapo, ukiangalia Vee Money ni mtu wa kutumia fursa, akipata ‘chaneli’ lazima ajiongeze. Diamond Platnumz alifanikiwa kuwashirikisha P Square katika Wimbo wa Kidogo haijakaa sana Vee Money akaibuka na kutoa Wimbo wa Kisela akiwa ameshirikiana na pacha wa P Square aitwaye Peter Okoye ‘Mr. P’. Huenda Jux anazubaa, wakati mwenzake akiiangalia fursa na kuzifanyia kazi yeye anabaki kukomaa na muziki wa nyumbani.
NI WOGA
Ukijaribu kuangalia Vee Money amekuwa karibu na wasanii wengi wa nje ya nchi, alishawahi kuwa kwa ukaribu na K.O hadi akatoa naye Wimbo wa Nobody But Me na kumuimbisha Kiswahili, vilevile alishawahi kuwa karibu na Orez, Reekado Banks, Ice Prince wote wa Nigeria pamoja na AKA wa Afrika Kusini ‘Sauz’ lakini kwa Jux huenda anaogopa kuwa karibu na watu hao akihofia kapo yake na Vee Money kwa maana ya wivu.
NI KURIDHIKA
Vee Money ni mwanamuziki pekee wa kike kufanya shoo kibao nje ya nchi zikiwemo Marekani, Kenya, Afrika Kusini, Uingereza, Nigeria na nyingine kibao.
Aprili 4, 2015 alishawahi kufanya bonge la shoo katika Tamasha la Gidi Culture ambalo ni tamasha kubwa la ufukweni kwa nchini Nigeria, Vee Money pia aliwahi kuitwa katika jointi ya pamoja na mastaa wenzake afrika kuimba wimbo wa pamoja akiwa na Victoria Kimani (Kenya), Judith Sephuma (Afrika Kusini), Waje (Nigeria), Arielle T (Gabon), Gabriela (Msumbiji), Yemi Alade (Nigeria) na Selomor Mtukudzi (Zimbabwe).
Shoo zote hizo, Jux amekuwa karibu kimahusiano na Vee Money lakini hajawahi kuonekana kuwa naye karibu kwenye matamasha hayo.
Kolabo zake ndani ya nchi alizozifanya na G Nako (Go Low), Ben Pol (Nakuchana), Stamina (Alisema), Joh Makini (Looking for You) zimemfanya kuridhika na kujiona bonge la msanii wa ndani ya nchi.

NI USHAMBA
Si kwa maana mbaya lakini kitendo cha kuziona fursa mbele yake, kitendo cha kutoweka ushindani nje ya nchi mfano wasanii wengi wamemkuta na sasa kidizaini f’lan kama wameshampita.
Mfano Harmonize aliyetoka mwishoni mwa 2015 alimkuta Jux kwenye gemu na sasa ukitaja wasanii Bongo wanaotambulika nje ya nchi huwezi kumuacha. Harmonize ameshafanya kolabo za kimataifa na Korede Bello (Nigeria), Sarkodie (Ghana), Eddy Kenzo (Uganda) na juzi kati Dar Live aliweka wazi tayari ana kolabo na Wizkid (Nigeria).
Ukija Rayvanny naye amemkuta Jux lakini tayari ana kolabo moja kibindoni akimshirikisha Rapa Khaligraph (Kenya).
NOEL JOSEPH.