
HATIMAYE Simba ya msimu ujao itakuwa hatari, hiyo ni baada ya kuonekana kuwa imekamilika kila sehemu na uhakika ni kwamba timu hiyo inaweza kuwa na vikosi vitatu na vyote ni moto. Simba jana ilikamilisha usajili wa mshambuliaji hatari Afrika Mashariki na Kati, Meddie Kagere, lakini ilitajwa pia kuwa inaweza kumpa mkataba beki mahiri, Pascal Wawa muda wowote kuanzia jana.
Ukiachana na hao, Simba tayari imeshawasajili wachezaji wengine watatu mahiri, mshambuliaji Adam Salamba kutoka Lipuli, Mohamed Rashid (Prisons ) na Marcel Boniventure Kaheza wa Majimaji, ukiongeza Wawa na Kagere, tayari mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wameshasajili wachezaji watano.
Hii inaonyesha kuwa Simba ambayo msimu uliopita ilipoteza mchezo mmoja tu kwenye ligi, inaweza kufanya mambo makubwa msimu ujao kuliko msimu uliopita ambao ilitwaa ubingwa. Kutokana na usajili huo, Simba sasa inaweza kuwa na vikosi vitatu ambapo kila kimoja kitakuwa pasua kichwa.

“Hatutaki mtu atusumbue msimu ujao, kama mchezaji atakuwa staa atakaa jukwaani, tumechoka kuchezewa,” kilisema chanzo cha habari kutoka kwenye benchi la ufundi la Simba.
Kutokana na usajili huo, kikosi cha kwanza cha Simba kinaweza kupangwa kwa mfumo wa 4-42 na kuwa hivi; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Asante Kwasi, Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere.
Hata hivyo, kocha wa Simba anaweza kuamua kwenye mchezo mwingine akapanga mashine zake kwa mfumo wa 4-3-3 ambapo atawapumzisha wachezaji wachache ambapo kikosi kinaweza kuwa hivi; Kipa Said Mohammed ‘Nduda’, mabeki Kapombe, Wawa, Nyoni, Mohamed Hussein Zimbwe, Mzamiru Yassin, James Kotei, Jonas Mkude, Kichuya, Bocco na Kagere.
Lakini wakati atakapotaka kutumia mfumo wa 3-5-2, kwenye mchezo rahisi aidha wa ligi au Kombe la FA, kocha wa Simba anaweza kuwapanga wachezaji wake hivi: Ally Salim, Yusuf Mlipili, Paul Bukaba, Salim Mbonde, Kichuya, Nyoni, Said Ndemla, Mohammed Ibrahim, Kaheza, Salamba na Mohamed Rashid.
Vikosi vyote hivi vya Simba, vinaonyesha kuwa ni moto wa kuotea mbali na vinaweza kumpasua kichwa kocha wa Simba kuhakikisha kuwa anawatumia wachezaji wote kwenye kikosi chake.
Lakini hii inaonyesha kuwa Simba watakuwa na wanaume wa kweli na hata kama akitoka mchezaji mmoja na kuingia mwingine basi moto unakuwa uleule. “Tunataka timu ambayo haiwezi kupata shida kama mchezaji mmoja ataumia, hii itatusaidia hata wakati ambapo kuna mchezaji anasumbuliwa na majeraha basi mwenzake anaweza kuziba pengo lake.
“Lakini pia tunataka kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ndiyo maana unaona tunawasajili wachezaji wengi wenye uzoefu na michuano hiyo.
“Ukiangalia wachezaji kama Wawa, Kagere halafu tuna Okwi na Bocco wote wana uzoefu wa kutosha kwenye michuano ya kimataifa, hivyo hatuwezi kupata shida, msimu uliopita tulishindwa kupata matokeo mazuri kwenye michuano ya kimataifa kwa kuwa hatukuwa na wazoefu kwenye kikosi,” alisema kiongozi mmoja ambaye yupo kwenye kamati ya usajili ya Simba.
Simba inalazimika kuwa na kikosi kipana zaidi kwani hivi sasa inajiandaa na michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza keshokutwa Ijumaa, lakini pia msimu ujao ukiondoa Ligi Kuu Bara na Kombe la Mapinduzi ambalo hufanyika kila mwaka, Simba itashiriki pia Ligi ya Mabingwa Afrika.