
MAISHA ya muuza nyago kwenye video za Kibongo, Tunda kwa mashabiki au watu wanaomfuatilia ni sanaa, halafu wakati huohuo ni mtihani, tena wenye maswali milioni ambayo wakati mwingine unaweza kujiuliza na usipate majibu.
Mfano wa maswali hayo ni hili; ‘life’ yake anayotuonyesha kwenye mitandao ya kijamii kwa picha za bandika-bandua akiwa sehemu tofautitofauti, kama ufukweni, hotelini, klabu na sehemu mbalimbali za starehe ni bata tu au ni kazi?
Kama ni bata basi anakula bata za maana mpaka kuku anaona wivu! Lakini, swali la kujiuliza nani yupo nyuma ya bata hizo? Ni kazi yake, mpenzi wake, kampuni au kitu gani?

TUANZE NA KAZI
Tunda ni mwanamitindo kama ambavyo amejitambulisha kwenye mtandao wa kijamii wa ‘Instagram’. Ni kweli ukichungulia kwenye sifa ya kuwa mwanamitindo anayo, anaingia kwenye kipengele cha muuza sura kwenye video ‘video vixen’, ingawa anaonekana kwa nadra kwenye video hizo.
Sasa, kwa video anazofanya zinamtosheleza kupata kipato cha kula bata hizo? Jibu ni hapana. Kwa nini hapana? Kwa sababu, wengi wetu tunafahamu kwamba mavideo vixen Bongo, hawalipwi hata zaidi ya laki mbili kwa video moja.
Kina Amber Lulu na Gigy Money, tuliwasikia mara kadhaa huko nyuma wakilia kushutishwa video kisha kuambulia shilingi 20,000, tena hapo wamefanya kazi na wasanii wakubwa kama Nay wa Mitego na Harmonize.
Ikafikia hatua warembo hao wakiwemo kina Lulu Diva, Kim Nana, Erycah na wengine wengi kutimua mbio na kuitelekeza tasnia hiyo kisa maslahi na kwa sasa wanafurahia maisha wakiwa wanamuziki.
Sasa ukitazama bata za Tunda za kila siku ambazo anaposti kwenye mitandao ya kijamii utaona wazi kwamba kazi yake haimuingizii kipato cha kutesa kwa bata hizo, maana video moja anaweza kushuti hata baada ya miezi sita kupita.
MPENZI WAKE
Tunda anasemwa kutoka kimapenzi na Casto Dickson, Mtangazaji wa Clouds Televisheni. Je, huyu ndiye anaweza kuwa anasimamia ‘shoo?’
Ukijiuliza hili swali, inabidi pia kurudi kwenye ukweli kwamba Tunda, hajaanza bata jana wala juzi. Kitambo tu anakula bata. Hata kabla ya Casto, kipindi yupo na Young Dee na wapenzi wake wengine alikuwa ni mtu wa bata.
Tukianza nyuma, Young Dee, alikwishawahi kuweka wazi hahusiki na maisha ya bata ya Tunda. Hata Casto, kuna uwezekano mkubwa hahusiki na bata hizo, kwa sababu kwanza, kama mpenzi wake, kama angekuwa na shoo kuna uwezekano mkubwa wangekuwa wanaonekana pamoja.
Lakini Tunda mwenyewe amekwishaweka wazi na kusema kwamba bata zake zinatokana na michongo yake!
MICHONGO IPI?
Hili nalo ni swali zuri kabisa la kujiuliza. Kumbuka Tunda anajiita pia ‘Boss babe’, akimaanisha ni mwanadada bosi- mwenye pesa yaani! Tukirudi kwenye michongo yake, swali ni kwamba ni michongo ipi hiyo anayofanya mbali na kuwa video vixen? Ukimuuliza haweki wazi! Kwa hiyo michongo yake ni ya siri si ndiyo. Inawezekana kwenye hizo bata anazokula kutokana na michongo yake pengine anakuwa kazini au wewe unawaza nini? Ukweli ni kwamba jibu lake linaacha maswali mengi!
MADAI YA KUWA MUONGO
Madai haya yanamuandama Tunda. Unajua Tunda, media nyingi na waandishi wengi tunamfahamu kama Tunda Sebasita ndiyo jina lake la kuzaliwa. Lakini kuna madai kwamba si jina lake halisi, jina lake ni Anna Patrick Kimario, kwamba baba yake ni mtu wa Arusha na Tunda alisomea Morogoro.
Ukimuuliza juu ya hayo, Tunda huwa hapendi kuzungumzia. Kwa hiyo, unaweza kuona mambo mengi kwenye maisha ya mwanadada huyu mrembo ambaye anapendwa na wengi yanaacha utata na maswali milioni.
Makala: BONIPHACE NGUMIJE