



…Akimkabidhi rasmi vyoo Mjema.

MKUU wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema amekabidhiwa vyoo vya kisasa vyenye matundu 12 kwa Shule ya Msingi Kivule, Wilaya ya Ilala, ambavyo ni maalum kwa wanafunzi wa kike.
Vyoo hivyo vimejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Total Tanzania kwa lengo kuu la kupunguza adha walizokuwa wanazipata hasa watoto wa kike nyakati za siku zao kwani vina kila aina ya huduma kwa ajili yao.
Pamoja na kuisifia kampuni hiyo na kuitia moyo ili iendelee kuisaidia wilaya yake, Mjema pia ameamuru watu waliohusika na wizi wa vifaa vya ujenzi wa vyoo hivyo, wachukuliwe hatua mara moja.
Wakati huohuo, akizungumzia hali ya maendeleo ya shule, alitoa onyo kwa waonyesha sinema (vibanda-umiza) wakati wa mchana na wakati wa masomo, waache tabia hiyo, kwani wanachangia katika kusababisha utoro shuleni na kuchochea tabia mbaya kwa wanafunzi kwa kutazama picha chafu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Total, Tarik Moufaddal, amesema wametenga shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali ambapo wanafanya hivyo maeneo tofauti ukiwamo mkoa wa Singida.
Aliongeza kwamba kampuni yake ina zaidi ya miaka 45 hapa nchini na imekuwa ikishiriki katika kusaidia jitihada za serikali kuboresha maisha ya wananchi, miundombinu na miradi mingine ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kwa wajasiriamali ili wajiendeleze katika shughuli za kimaendeleo.