
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akizungumza na waandishi wa habari.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kujisalimisha kwa mkuu wa polisi mkoani Lindi ili achukuliwe hatua stahiki kwa madai ya kufanya uchochezi kwenye jimbo la Kilwa dhidi ya Mbunge Said Bungara.

Lugola amesisitiza kwamba iwapo Zitto hatajisalimisha ndani ya siku mbili, atamwamuru Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amkamate popote alipo.
Pia amemtaka Sirro amchukulie hatua mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilwa kwa kutomchukulia hatua Zitto na amesema kwamba hakuna mtu atakayepona kwenye kampeni iwapo maneno ya uchochezi yatatumika.
Hata hivyo, baada ya kutakiwa kujisalimisha, Zitto Kabwe amemjibu Lugola kupitia akaunti yake ya Twitter kwamba:
“Waziri hana hayo mamlaka. Kama polisi wananitaka watoe wito wa kisheria nitakwenda. Naendelea na kampeni za Mbunge wa Buyungu ambapo tunamwunga Mgombea wa Chadema na madiwani wa ACT Wazalendo kwenye kata kadhaa. Nashauri Waziri ampate kwanza yule Mbwa wa Polisi Bandari”
