
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha cha Texas A&M nchini Marekani, Makenzie Nolan, alihakikisha kuwa picha za sherehe yake ya kufuzu zitakuwa za kukumbukwa baada ya kupigwa picha na mamba wa urefu wa mita nne.
Makenzie Noland ambaye amehitimu shahada katika masuala ya sayansi ya wanyama wa porini na viumbe wa majini mwezi Aprili mwaka huu, amekuwa akipata mafunzo kwenye kituo cha kutunzia wanyama cha Beaumont ambapo ni eneo la makazi ya mamba 450 na wanyama wengine.

Makenzie na mamba mmoja anayejulikana kwa jina la Tex, wamekuwa na uhusiano maalumu tangu ajiunge na kituo hicho.
Anasema mamba huyo huitikia jina lake na ishara za mikono yake anapoingia kwenye kidimbwi kumlisha.
“Ninaingia kwenye kidimbwi chake kila siku, ni rafiki yangu mkubwa,” aliiambia BBC.
Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21, alikulia huko Bellevue, Nebraska, ambapo kumuona mamba ni ndoto lakini kwa sasa anawahudumia mamba kila siku.
“Tangu nikiwa mdogo nilikuwa nashika nyoka na wanyama wengine,” anasema.
Alitarajia picha hizo zingeonyesha kile ambacho amekuwa akifanya msimu wa joto akiongeza kwamba amefurahishwa na maoni ya watu kutokana na picha zake ambazo zimesambazwa mara nyingi.
“Sikutarajia hili; lengo langu lilikuwa ni kuchapisha picha nzuri kwenye Instagram,” anasema kwa kumalizia na kuahidi kuendelea kufanya kazi na sekta ya wanyamapori baada ya kufuzu.