×

Mwanariadha wa Kenya Nicholas Bett Afariki

MWANARIADHA wa Kenya, Nicholas Bett, bingwa wa dunia wa mbio za mita 400 kuruka viunzi wa mwaka 2015, amefariki dunia kwenye ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Lesso, Jimbo la Nandi, katika eneo la Bonde la Ufa.

Bett amefariki papohapo baada ya gari alilokuwa akiendesha kupoteza mwelekeo baada ya kugonga tuta la barabarani na kusababisha gari hilo kutoka barabarani na kuingia kwenye shimo.

Ajali hiyo ilitokea karibu na eneo la Lessos katika barabara ya Eldoret- Kapsabet kaunti ya Nandi.

Kamanda wa polisi eneo hilo, Partrick Wambani, amethibitisha kifo hicho na kusema matayarisho ya kuupeleka mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti yanaendelea.

Bett ambaye alikuwa katika timu ya Kenya ambayo ilishiriki mashindano ya riadha ya Bara Afrika yaliyotamatika hivi punde huko Asaba nchini Nigeria,  alikuwa akirudi nyumbani kutoka jijini Nairobi.

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala ya rambirambi kwa jamaa, ndugu na marafiki wa aliyekuwa bingwa wa dunia katika mbio za mita 400 za kuruka viunzi ambaye alifariki leo katika ajali ya barabarani.

Katika risala hiyo, Rais Kenyatta amesema amehuzunishwa sana na kifo cha mwanariadha huyo ambaye alililetea taifa hili sifa nyingi kutokana na ushindi wake katika ngazi za kimataifa.

“Kwa hakika inahuzunisha sana kwamba tumempoteza mwanariadha shupavu katika ajali ya barabarani. Natoa pole zangu za dhati kwa familia, ndugu na marafiki wa marehemu Nicholas Bett,” alisema Rais Kenyatta.

Rais aliongeza, “Naungana na wanariadha katika kumuomboleza Nicholas Bett ambaye ni bingwa wa mwaka wa 2015 katika mbio za mita 400 kuruka viunzi, na ambaye amefariki kutokana na ajali ya barabarani huko Lessos, kaunti ya Nandi. Mwenyezi Mungu aifariji familia, ndugu na marafiki wa shujaa huyu.”

Bett alirejea nchini jana kutoka kwa mashindano ya Bara Afrika yaliyofanyika nchini Nigeria.

Alikuwa miongoni mwa wanariadha wa timu ya taifa iliyoshiriki katika mashindano hayo yaliyomalizika hivi punde huko Asaba, Nigeria.

Sifa za Bett zilienea kimataifa aliposhinda mbio za mita 400 kuruka viunzi katika mashindano ya Shirikisho la Kimataifa la Wanariadha (IAAF) yaliyofanyika jijini Beijing, China, mwaka wa 2015, hii ikimfanya kuwa Mkenya wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mbio za masafa mafupi katika ngazi za kimataifa.