
WAKATI Man City wakitoka sare ya bao 1-1 na Wolves, Arsenal wenyewe walirudi kwenye mbio za ushindi baada ya kuwachapa West Ham mabao 3-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa jana Jumamosi kwenye Uwanja wa Emirates jijini London. Huu umekuwa ushindi wa kwanza wa Arsenal msimu huu, baada ya kufungwa michezo
michezo miwili ya kwanza ya msimu.
Arsenal walichapwa na Man City 2-0 nyumbani na kulizwa 3-2 ugenini na Chelsea, lakini West Ham hali ndio mbaya zaidi kwani wamepoteza mchezo wao wa tatu mfululizo.

Kocha Unai Emery, jana alikuwa na furaha ya kuonja ushindi wa Ligi Kuu England baada ya Arsenal kufunga bao la kwanza kupitia kwa beki wake Nacho Monreal ambaye alifunga kwa shuti kali katika dakika ya 30 ya mchezo likiwa ni la kusawazisha baada ya Marco Arnautovic, kuanza kuifungia West Ham katika dakika ya 25.
Arsenal walijipatia bao la pili kwenye mchezo huo katika dakika ya 70 baada ya Issa Diop kujifunga. Katika dakika ya 90, Danny Welbeck aliifungia Arsenal bao la tatu ndani ya 18, huu ukiwa ushindi wao wa kwanza msimu huu. Man City ambao walikuwa wameshinda michezo yao yote miwili ya mwanzo walijikuta wakiambulia sare dhidi ya Wolves.

Wolves ambao walikuwa nyumbani kwenye uwanja wa Molineux, walianza kujipatia bao kupitia kwa Wily Boly katika dakika ya 57, huku City wakisawazisha kupitia kwa Aymeric Laporte katika dakika ya 69. Sasa Man City wana pointi saba katika michezo mitatu na Arsenal wana pointi tatu katika michezo mitatu.