
SIMBA imeanza Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons. Hii mechi ilipigwa kwenye Uwanja wa Taifa usiku wa Jumatano baada ya ubwabwa wa sikukuu. Lakini haya matokeo ni kama vile hayakuwafurahisha mashabiki na wadau wa Simba.
Yameibua maneno mengi kwenye mitandao ya kijamii ambayo yanaashiria kwamba waliingia uwanjani na matokeo yao au walikuwa wanatazama mechi vibandani wakiwa na matokeo wanayoyajua wao. Kuna picha inasambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha lori limebeba mashabiki wa Prisons lakini Simba wanadai wale ni wachezaji wakiingia kwenye Uwanja wa Taifa siku ya mechi.
Ni aina fulani ya upotoshaji unaofanywa kuaminisha wadau kwamba ‘tunashindaje goli moja dhidi ya timu inayokuja uwanjani kwa lori?’ Aina ya kikosi kilichosajiliwa na Simba kinawapa kiburi mashabiki wao, lakini wanasahau kwamba wanapaswa kuziheshimu timu nyingine.

Ni raha ya shabiki timu yake kusheheni mastaa wakubwa kwenye mchezo husika kutoka sehemu mbalimbali, lakini hiyo siyo tiketi ya moja kwa moja ya kupata matokeo.
Lazima tujifunze kuheshimu timu pinzani, hii ni soka na matokeo yanatokana na kile unachokifanya ndani ya dakika 90. Haya maneno mengine ya nje ya uwanja ni mbwembwe.
Mashabiki na wadau waache kocha na wachezaji wafanye kazi yao uwanjani. Ishu ya Simba kuweka kambi Uturuki, Prisons kuweka Tukuyu au Yanga kukaa Kilosa ni sehemu ya maandalizi tu, ambayo mwisho wa siku hayahusiani moja kwa moja na kile kitakachotokea uwanjani.
Mchezaji anaweza kukaa kambini sehemu tulivu akapata kila kitu lakini mwisho wa siku kutokana na uzito wa mwili au ugumu wa mazoezi aliyokuwa anapata ikamchukua muda kutoa matokeo chanya uwanjani ambayo mashabiki wanayo vichwani mwao. Ishu ya msingi kwenye ligi haswa katika hatua za kwanza kama ilivyo sasa ni pointi. Magoli siyo ishu sana, Simba wabadilike wajifunze kuziheshimu timu nyingine.
Hata wangeifunga Prisons mabao 20 bado pointi zingekuwa ni zilezile tatu tu. Na lazima watambue kwamba Prisons siyo timu mbovu, ni timu ambayo ina wachezaji wengi vijana wenye uchu wa mafanikio na wenye nidhamu ya mchezo ambao wamekaa pamoja kwa muda mrefu.
Prisons inacheza kitimu zaidi iheshimiwe kama mpinzani, waliokuwa wanafuatilia ule mchezo haswa kipindi cha pili waliona Prisons ilichofanya. Siyo timu ya kubeza au ya kwenda uwanjani ukiwa na matokeo yako mfukoni. Tujifunze kuheshimu kazi za watu wengine.
Mashabiki wampe muda Kocha wa Simba afanye kazi yake, yule wa Prisons amekaa muda mrefu sana na timu yake na hata msimu uliopita alifanya vizuri na kuwa kocha bora.
Ligi ndiyo kwanza inaanza mashabiki waache papara na maneno ya kukatisha tamaa wachezaji, wawape morali tuone ligi ya maana na soka lenye ushindani. Bado safari ni ndefu, jifunzeni kuheshimu wapinzani.
NA MZEE WA KUTIBUA