
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amemweka ndani Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Mtwara (OCS) Ibrahim Mhando, kwa kushindwa kuwaweka mahabusu watuhumiwa wanne.
Kati ya watuhumiwa hao yupo Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Y&P Architects, Benjamin Kasiga, ambaye anadaiwa kutoa taarifa ya uongo kwa waziri huyo kuhusu ujenzi wa ofisi ya Uhamiaji mkoani humo.
Waziri Lugola leo asubuhi Agosti 27, 2018 akiwa njiani kwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya safari ya kurudi Dar es Salaam alipita kwa kushitukiza katika kituo cha Polisi Mtwara mjini akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu.
Lugola alitaka kuthibitisha kama mtuhumiwa ambaye alielekeza jana usiku akamatwe awekwe mahabusu kama polisi walitekeleza agizo lake.
Baaada ya kufika kituoni hapo alimkuta mtuhumiwa huyo akiwa chumba cha upelelezi badala ya kuwekwa mahabusu ya polisi, hivyo akamuuliza kamanda wa polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya, sababu za kutotekelezwa agizo lake.
“Hivi ndivyo polisi mnafanya hivi, haya ndiyo madudu mnayoyafanya? Tabia hii siku zote tunaipinga ikichafua polisi na hii ndiyo tabia yenu. Najua ndiyo mana nimekuja ghafla, mnafahamu maadili ya jeshi?”
“RPC hawa polisi wako wanafanya nini? OCS njoo hapa, kwa nini umeweka hawa watuhumiwa chumba cha upepelezi badala ya mahabusu, nawe unaingia ndani kwa kushindwa kuwaweka ndani hawa watuhumiwa. RPC muweke ndani sasa hivi huyu,” aliamuru Lugola.
Hata hivyo, Mkondya amemweleza Lugola kuwa polisi wake walifanya makosa kwa kutowaweka mahabusu watuhumiwa hao.