
JANGA alilochuma mtangazaji ambaye pia ni mwigizaji wa Bongo Movies, Burton Mwamba ‘Mwijaku’ kwa kujitangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa yeye ni baba wa mtoto wa Tanasha Donna, huwenda akalila na nduguze.
Taarifa kutoka duru za kisheria, zinaonesha kuwa mtangazaji huyo, anaweza kubanwa kisheria na kulazimika kumlipa Tanasha mamilioni ya fedha, kufungwa jela au vyote kwa pamoja.
Hii inakuja siku chache baada ya Tanasha ambaye amethibitisha baba wa mwanaye kuwa ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ kuonesha nia ya kumburuza Mwijaku mahakamani.
“Muda mfupi ujao, Mwijaku atapokea barua kutoka kwa wakili wangu.”
Tanasha aliandika hayo kwenye Insta Story ya ukurasa wake wa Instagram baada ya kushauriwa kuchukua hatua hiyo na watu wake wa karibu akiwemo mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’.
MASHTAKA YANAYOMKABILI MWIJAKU
Endapo azma ya Tanasha kumchukulia hatua Mwijaku itakuwa na mashiko, basi huwenda mwanasheria wake akatumia aina mbili za makosa.
Kwa mujibu wa mwanasheria Emmanuel Elias, makosa hayo ni jinai au madai ambayo yote yanaangukia kwenye tuhuma za Mwijaku.
“Kama mahakama itathibitisha kuwa mtangazaji huyo kasema uongo katika madai yake, atakuwa amefanya kosa kisheria.
“Kwa kuwa hatufahamu ni aina gani ya madai yatawasilishwa mahakamani, lakini mwanga uliopo kisheria upo kwenye aina hiyo ya makosa niliyotaja.
“Tafsiri ya makosa haya inapatikana kwenye sheria mbili, ya kwanza ni ile ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, yaani ‘The Cyber Crimes Act. No 4 of 2015’.
“Nyingine ni Sheria ya Vyombo vya Habari ‘The Media Services Act. No. 15 of 2016, ambapo ile ya kwanza itatumika kwenye jinai na hii ya pili itatumika endapo kuna udhalilishaji katika madai ya Mwijaku,” alisema mwanasheria Emmanuel.
KUHUSU ADHABU
Mwanasheria huyo alisema kuwa, kuhusu adhabu endapo mtuhumiwa atakuwa na hatia kwenye jinai kwa kusambaza maudhui yenye uovu kwa mlalamikaji na Sheria ya Makosa ya Mtandao ikatumika, atahukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni tatu au kwenda jela kwa miezi sita au adhabu zote kwa pamoja.
Alisema kuwa, mahakama ikitumia sheria ya habari, mtuhumiwa atalazimika kumlipa mlalamikaji faini isiyopungua shilingi milioni tano na isiyozidi milioni 20.
Emmanuel aliongeza kuwa, endapo mtuhumiwa akishindwa kulipa faini hiyo, atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.
KUHUSU MADAI
Akifafanua zaidi kuhusu uwezekano wa mtuhumiwa kutakiwa kumlipa mlalamikaji fidia itokanayo na udhalilishaji (defamation), mwanasheria huyo alisema;
“Mara nyingi kwenye fidia mlalamikaji ndiye ambaye huwa anaomba mahakama kulipwa kiasi ambacho yeye anaona anastahili.
“Ndiyo maana umesikia kuna wengine wanaomba fidia ya shilingi milioni mia tano, wengine milioni mia mbili na wengine shilingi milioni moja kama alivyofanya Yusuf Manji kwenye kesi yake na marehemu Dk Reginald Mengi.
“Kazi ya mahakama huwa ni kupima uzito wa madai na hadhi ya mdai mwenyewe, kisha hupendekeza kiasi cha fedha kwenye hiyo fidia aliyoomba mlalamikaji.
“Suala la umaarufu wa mtu huwa ni msingi wa uamuzi, kumlipa fidia mtu ambaye siyo maarufu, huwa ni rahisi kuliko mtu maarufu kama mbunge, waziri au kiongozi yeyote kwenye jamii,” alisema Emmanuel.
MWIJAKU AWA GUMZO
Kutokana na madai ya Mwijaku ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara kuwa mtoto wa Tanasha ni wake, yamemfanya mtangazaji huyo kugeuka gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Jicho la mwandishi wetu lililopita kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii lilibaini kuwa, msingi wa mjadala umejengwa kwenye nia ya mtangazaji huyo kujitangazia ubaba wa mtoto.
“Huyu jamaa (Mwijaku) ni mtu wa sifa, lakini kujitangazia kuwa yeye ni baba wa mtoto wa Tanasha, ni ujasiri uliopitiliza, hasa ikiwa si kweli,” mmoja aliandika komenti yake kwenye Mtandao wa Instagram.
Mwingine alisikitishwa na madai hayo kwa kusema yana udhalilishaji mkubwa kwa mtoto, baba na mama yake.
“Huyu jamaa huwaga simwelewi kabisa, unajua unaposema mtoto ni wako, ina maana baba wa mtoto aliyetajwa anakuwa kasingiziwa, maana yake nini?
“Haiishii hapo, mama wa mtoto unakuwa umempa tuhuma kuwa alichepuka na huyo mtoto akikua na kuja kukutana na video zako za kudai wewe ndiye baba yake, unadhani atajisikiaje?
“Kuna mambo mengine yanahitaji akili sana, siyo matope kama ya huyu mshikaji,” mwingine aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Hata hivyo, ukakasi wote ambao umekuwa ukitolewa na baadhi ya watu, umekuwa haumshtui Mwijaku na kujikuta akirudia mara kwa mara madai yake.
Ujasiri huo ndiyo ambao umewafanya baadhi ya watu kuamini kuwa huwenda anachokisema ana uhakika nacho, hivyo kufanya mahakama ambayo itapewa jukumu karibuni kubaki mteguzi wa kitendawili hiki chenye utamu unao kolea.
STORI: Mwandishi Wetu, Risasi