
IJUMAA Sexiest Girl 2015 ndiyo iliyonifanya kufahamiana na muuza nyago kwenye video za Bongo Fleva, Gift Stanford ‘Gigy Money’ kwani alikuwa ni mmoja wa washiriki.
Nakumbuka wiki moja baada ya kumalizika kwa shindano hilo lilioendeshwa na moja kati ya magazeti kongwe ya Global Publishers ‘Ijumaa’ ambapo Asha Salum ‘Kidoa’ aliibuka mshindi, nilikutana na Gigy kuzungumza mengi kuhusiana na kipaji chake cha kuimba na kuuza nyago.
Hakuwa Gigy wa kwenye chati kipindi hicho, wauza nyago Tunda, Zuhura Gora, Baby Nahiyyah, Haitham, Kidoa na wengine wengi walikuwa ‘wanamkalisha’, alikuwa ndiyo kwanza ameanza maisha ya kujitegemea baada ya kuachana na muuza nyago mwenzake, Lulu Euggen ‘Amber Lulu’ waliokuwa wakiishi gheto moja.
Kutokana na wauza nyago hawa kila mmoja kufanya maisha yake baada ya kuona kazi hiyo hailipi, ndipo mwanya ulipojitokeza kwa Gigy, Amber, Kim Nana, Nai, Lulu Diva na wengineo kuchipukia na kuanza kusumbua kwenye muziki.
Ukiweka pembeni hilo, kwa muda mrefu Gigy amekuwa na sarakasi za hapa na pale katika maisha yake ndani na nje ya muziki, amekuwa akifosi kupata ‘tension’ kwa mashabiki kwa kuachia picha za nusu utupu au kufanya kituko cha ‘aibu’, kwake kujilipua katoka na staa haoni shida, kama utakumbuka alishawahi kuanika kutoka kimapenzi na baadhi ya masta Bongo akiwemo Rich Mavoko.
Alishawahi tena kumchana Nay wa Mitego kudai kuwa amemtapeli kwenye video ya Wimbo wa Shika Adabu Yako na kusema kuwa aliambulia shilingi elfu ishirini tu. Lakini pia, ndani ya mwaka huu tu, amefanya vituko vingi vya kushangaza na huenda ni msanii pekee kuwahi kufanya hivyo tangu tasnia hiyo ianzishwe. Star Showbiz limekunyumbulia baadhi tu ya hayo;
WAZIRI SHONZA AMUITA
Alianza Januari, mwaka huu ambapo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alimuita ofisini kwake akidaiwa kutumia mitandao ya kijamii hovyo kwa kuweka picha za nusu utupu. Katika hili, alionekana kutii na kufika basata akiongozana na mpenzi wake ambaye ni mtangazaji wa kituo kimoja cha redio nchini, Mourad Alpha ‘Moj’.Baada ya kutoka basata, Gigy aliangua kilio na kusema;
“Kila mtu na nyota yake wengine hawajaitwa kwa sababu hawajaonwa, hata nikiulizwa picha (za nusu utupu) nilizoposti hivi karibuni hakuna. Mtu kama mimi naona kama naonewa, naposti mwezi hadi mwezi, nina mimba ya miezi saba na hakuna aliyeiona mtandaoni. Kwanza sikutaka mtu yeyote aelewe nina mimba, sasa wameshanitoa kila mmoja anajua.”
KUMKANA BABA MTOTO
Mwezi mmoja baada ya kujifungua mtoto wa kike aitwaye Mayra, Giggy alifanyiwa mahojiano na kituo kimoja cha TV na kusema kuwa mpenzi wake aliyekuwa naye, Moj si baba wa mtoto. Ikumbukwe kuwa, tangu alipokuwa na ujauzito alikuwa anaishi na Moj na mashabiki wake wengi walikuwa wakilifahamu hilo.
Katika mahojiano hayo, Gigy alimwekea zigo la lawama Moj kuwa wakati ana ujauzito hakutaka kuishi naye na kumpa sababu nyingi, akadai kuwa ilifika wakati anampatia shilingi elfu moja ‘buku’ ya matumizi. Mwisho akasema baba wa mtoto anamjua mwenyewe na kwamba Moj si baba kama wengi wanavyodhani.
ADAI KUCHUMBIWA ZANZIBAR
Wakati akiwa ameshaweka sawa na Moj na kudai kuwa aliamua kuongea kwa hasira kuhusu baba halisi wa mtoto wakaendelea kuishi pamoja kama zamani, hivi karibuni limeibuka tena mitandaoni baada ya kusambaa picha zimuonesha akiwa katika mapozi tata na mwanaume mwingine.
Gigy ndiye aliyeweka picha hizo kwenye ukurasa wake wa Instagram zinazomuonesha akiwa na mwanaume kutoka visiwani Zanzibar na kudai kuwa amechumbiwa naye kwa hiyo ndoa itakuja hivi karibuni.
KUJIBEBISHA KWA MONDI
Kabla la mchumba kutoka Zanzibar halijapoa, juzikati ameonekana tena katika Ukumbi wa Samaki Samaki, Masaki jijini Dar kwenye bethidei ya kaka na DJ wa Diamond Platnumz ‘Mondi’, Romy Jones, Gigy alifanya kituko kingine cha ajabu sana.
Katika usiku huo, alishika kipaza sauti na kuanza kuimba wimbo wake wa Nampa Papa kisha akaanza kumgeukia Mondi na kuanza kumkatikia huku akionekana kumuangalia kimahaba. Kama hiyo haitoshi, alijiweka ‘close’ na Mondi na kumshikashika maeneno mbalimbali ya mwili wake.
MOJ ANASEMAJE?
Baada ya sarakasi hizo za Gigy zisizokuwa na ‘kichwa wala miguu’, nilimtafuta Moj ambaye ni mzazi mwenziye kujua kama bado wanaendelea kuishi pamoja ambapo hakuwa tayari kutia neno. “Ni bora kwanza atafutwe huyo jamaa ndipo na mimi nitaongea,” alisema Moj.
MAKALA: ANDREW CARLOS