×

MTAWA ALIJIRUSHA, ALIRUSHWA? MASWALI 6 MAZITO

Tukio la Mtawa Suzana Bartholomew ‘48’ (pichani), aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kudaiwa kujirusha kutoka ghorofa ya pili ya jengo la hospitali hiyo na kufa, limezua mjadala mkubwa nchini, hasa mitandaoni na kuibua maswali yasiyokuwa na majibu.

1: ALIJIRUSHA AU ALIRUSHWA?

Kufuatia vuta-nikuvute ya mijadala inayoendelea, baadhi ya watu walidai mtawa huyo hakujirusha na kukatisha maisha yake kama ilivyodaiwa na Jeshi la Polisi, bali huenda alirushwa kwa lengo la kukatisha uhai wake. Ingawa Jeshi la Polisi bado linafanya uchunguzi juu ya jambo hilo, Gazeti la Ijumaa liliamua kuzama ndani na kufanya uchunguzi ili kufahamu hasa ni kitu gani kilichotokea ili ukweli ujulikane.

Vyanzo mbalimbali vya habari vilivyozungumza na gazeti hili wakiwemo baadhi ya watawa kwa masharti ya kutotajwa, walidai kuwa kabla ya ajali hiyo, Sista Suzana alikuwa katika hali mbaya ya simanzi na kuchanganyikiwa iliyotokana na kuwepo kwa kutoelewana kati yake na mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Abel Makubi.

Chanzo kikubwa cha mgogoro huo kilidaiwa kuwa ni tuhuma nzito za mkurugenzi akimlalamikia mtawa huyo kwamba katika utendaji wake alikuwa akificha baadhi ya mapato ya hospitali.

Hospitali ya Bugando inaendeshwa kwa ubia kati ya Serikali ambayo huteua mkurugenzi ambaye husimamia uendeshaji na Kanisa Katoliki ambalo huteua mkurugenzi wa fedha kusimamia mapato, kazi iliyokuwa ikifanywa na Sista Suzana kabla ya kifo chake.

“Tuhuma hizi ziliibuka mara kwa mara katika vikao vya bodi, mkurugenzi akimtuhumu sista huyo kwa kutokuwa na uadilifu katika kazi hiyo na kusababisha upotevu wa mapato, jambo ambalo mtawa Suzana alilikanusha kabisa na kusababisha uhusiano wake na mkurugenzi kuwa mbaya,” kilieleza moja ya vyanzo vyetu.

Ilidaiwa kuwa kufuatia hali hiyo ya kutoelewana, sista Suzana alikuwa mtu asiye na raha na kazi yake na mara kadhaa alitamani kuacha kazi ili arejee Kagera yalipo makao makuu ya shirika lake la watawa wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, lakini alilazimika kuendelea na kazi baada ya kupokea ushauri kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo maaskofu wa Kanisa Katoliki waliomtaka asikate tamaa.

Pia iliendelea kudaiwa kuwa, kitu kingine kilichomchonganisha sista Suzana na mkurugenzi ni uamuzi wake wa kusisitiza mapato ya mkurugenzi yakatwe kodi na kufanya yaporomoke hadi shilingi milioni nne, jambo ambalo mkurugenzi huyo halikumfurahisha na kusababisha moto wa kutoelewana kati yao uwe mkubwa zaidi.

Ilidaiwa kwamba, miezi michache iliyopita, Idara ya Uhasibu ya Hospitali ya Bugando ambayo mtawa Suzana aliiongoza, ilipatwa na kashfa ya upotevu wa fedha uliotokana na baadhi ya wahasibu waliofanya kazi chini yake kufungua akaunti kwa siri na kuwa wanaelekeza sehemu ya mapato ya hospitali kwenye akaunti hizo.

“Jumla ya fedha zisizopungua shilingi milioni 300 zinadaiwa kupotea na wafanyakazi wa chini yake walikamatwa, wengine walisimamishwa kazi na wengine kufukuzwa,” alieleza mmoja wa wafanyakazi wa Hospitali ya Bugando.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa, kwa sababu ya cheo chake kama kiongozi wa idara, sista Suzana ilibidi awajibike ingawa hakuwa amehusika moja kwa moja na upotevu wa fedha hizo.

Ilisemekana kufuatia upotevu huo na kwa shinikizo la viongozi wa hospitali, mtawa Suzana na wenzake wanane walifikishwa Polisi na baadaye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambako upelelezi ulianza na kumsababishia mtawa Suzana hali mbaya kisaikolojia kwa sababu kama mtawa hakuzoea misukosuko ya Polisi na aliona hiyo kama kashfa kubwa katika maisha yake ya utawa.

Ilielezwa kuwa, baadaye usuluhishi ulifanyika kati ya uongozi wa hospitali na maaskofu ambapo iliamriwa kuwa sista Suzana apumzike kazi ya ukurugenzi wa fedha na kukabidhi kwa mtu mwingine kwani kwa hali ilivyokuwa, haikuwa rahisi kwa mkurugenzi wa hospitali na mtawa huyo kufanya kazi pamoja.

Uamuzi huo ulimlazimisha mtawa Suzana kuondoka Mwanza na kurejea Kashozi, Kagera yalipo makao makuu ya shirika lake la kitawa la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu.

Hata hivyo, Ijumaa ya Agosti 25, 2018, akiwa huko alidaiwa kupokea baruapepe kutoka kwa mkurugenzi wa hospitali iliyomtaka kurejea Bugando kwa ajili ya kuandaa ripoti ya kikao cha bodi ambacho kilitarajiwa kufanyika Jumanne ya Agosti 28.

Jumapili ya Agosti 26, alirejea Mwanza kama alivyoombwa na mkurugenzi, sababu ilikuwa ni siku ya mwisho wa wiki alidaiwa kusubiri mpaka siku ya Jumatatu ili akutane na uongozi wa hospitali kuzungumzia makabidhiano ya ziada ambayo yeye alidai kutoyafahamu kwani alishakabidhi kila kitu.

Ilifahamika kuwa, sista Suzana hakutoka kabisa ndani ya chumba chake tangu alipoingia, kiasi cha kuwafanya watawa wengine kuanza kuwa na wasiwasi na hali yake kwani wakati anaingia alionekana kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida.

“Siku ya Jumatatu alfajiri ndipo inadaiwa alipanda hadi ghorofa namba mbili ya jengo la Hospitali ya Bugando na kujirusha, tukio lililohitimisha maisha yake kabla hata hajaingia ofisini kuandika ripoti aliyotakiwa kuitayarisha kwa ajili ya bodi kwani watu aliokuwa amewakabidhi ofisi hawakuwa na uwezo wa kuitayarisha ripoti!” Kilidai chanzo chetu.

Aidha, habari nyingine ambazo gazeti hili limezipata zilidai kuwa, Polisi mkoani Mwanza walikubaliana na uongozi wa hospitali kuwa watafutwe wakaguzi wa hesabu ili waweze kupitia hesabu za hospitali hiyo kuthibitisha kama kweli palikuwa na ubadhirifu uliotokea au la.

Ilisemekana kwamba, jambo hilo liliibua mvutano kwani mkurugenzi wa hospitali alitaka wakaguzi wa nje ndiyo waifanye kazi hiyo, lakini maaskofu wakataka wakaguzi wa ndani, mvutano ambao ulifanya ukaguzi wa hesabu hizo ushindikane kufanyika na hivyo kushindwa kuthibitisha kama kweli wizi huo ulikuwa umetokea mpaka Agosti 28, mtawa Suzana alipopoteza uhai wake.

“Dunia nzima inalazimishwa kuamini kwamba sista Suzana alijirusha ghorofani na kufa kwa sababu ya upotevu wa fedha, jambo ambalo halina uhakika mpaka sasa, isitoshe hata kama upotevu huo utakuwepo haumhusu yeye moja kwa moja bali unamgusa kwa sababu ya uwajibikaji, hivyo si vyema hata kidogo kusema mtawa aliiba wakati wanaotuhumiwa kufungua akaunti na kupoteza fedha wapo, huku ni kutaka kumchafulia mtawa wa watu ambaye alijitoa maisha yake yote, akajinyima vitu vingi ili kumtumikia Mungu!” Alisema mmoja wa watawa ambaye ni mfanyakazi wa Hospitali ya Bugando.

Sista Suzana amefanya kazi na Hospitali ya Bugando kama Mkurugenzi wa Fedha kwa zaidi ya miaka kumi na kufanya kazi kwa mafanikio makubwa bila kashfa yoyote chini ya wakurugenzi wawili, Dk Mteta na Dk Majinge waliomtangulia mkurugenzi wa sasa, Dk Makubi.

Agosti 29, mwili wa sista Suzana ulisafirishwa kutoka Mwanza kuelekea Kashozi, Bukoba, yaliko makao makuu ya shirika lake kwa mazishi huku kifo chake kikiacha maswali mengi yasiyo na majibu baada ya simu yake moja kutoonekana, wakati iliyoonekana ilikutwa imechomolewa laini zote mbili. Baadhi ya maswali yanayoulizwa ni pamoja na;

2: SIMU, LAINI ZIKO WAPI?

Ilidaiwa kwamba mtawa huyo alikuwa na simu mbili, iliyoonekana ni moja ikiwa imetolewa laini zote mbili, je, nani aliyefanya hivyo na kwa sababu gani?

3: ALIWAHI KUUGUA UGONJWA WOWOTE?

Wananchi hao walitaka kujua kama kabla ya tukio hilo, je, sista Suzana aliwahi kuugua ugonjwa wowote ukiwemo malaria ambayo labda ilipanda kichwani? “Ukiacha kuumwa malaria, je, alikuwa na tatizo lolote la kisaikolojia au msongo uliosababisha kuchukua uamuzi huo ambao haujawahi kutokea kwa watawa?

4: Ni kweli chanzo ni ubadhirifu?

Swali lingine linaloulizwa na wengi ni je, ni kweli kwamba kujirusha kwake chanzo ni huo ubadhirifu wa pesa uliosemekana kutokea kwenye ofisi anayoisimamia au kuna lingine?

5: MARA YA MWISHO ALIWASILIANA NA NANI?

Swali lingine ni kwamba, kwa mara ya mwisho kwenye simu yake aliwasiliana na nani na je, waliongea nini? Mbali na simu, je, katika barua pepe au kurasa zake za mitandao ya kijamii alikuwa akifanya mawasiliano na akina nani na walikuwa wakizungumza nini?

6: ALIPOKEA VITISHO?

Wengine walihoji endapo sista Suzana alipokea vitisho vyovyote kutoka kwa mtu yeyote kupitia simu au mitandaoni?

KAMANDA ANASEMAJE?

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, ACP Jonathan Shanna akizungumza na vyombo vya habari juu ya tukio hilo alisema uchunguzi wa awali ulionesha kuwa ofisi aliyokuwa akiifanyia kazi kuna tuhuma za upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 300.

Alisema tuhuma hizo zilisababisha watumishi wenzake wanane kusimamishwa kazi na wengine kufukuzwa na yeye kukamatwa kisha akahojiwa na kuachiwa kwa dhamana.

Jitihada za kumpata mkurugenzi wa Bugando zilifanyika ambapo mwandishi wetu alifika hospitalini hapo na kukutana na mmoja wa maafisa habari ambaye alisema hataweza kumuona kiongozi huyo kwa kuwa maelezo yalishatolewa na Jeshi la Polisi. Hata hivyo, jitihada za kumpata kwa njia ya simu zilifanyika lakini hakuweza kupatikana hivyo juhudi za kumpata zinaendelea.

Wakati gazeti hili likienda mitamboni habari zilitufikia kutoka kwenye msafara wa maiti ya sista Suzana zilidai kuwa, ndugu wawili wa marehemu waliotajwa kwa majina ya Peter na Anthony gari lao lilizuiliwa na Polisi na kuhojiwa kuwa walipokuwa ICU (chumba cha uangalizi maalum) waliingia na bastola kwa nia ya kutaka kumdhuru mkurugenzi. Hata hivyo, waliachiwa baada ya mahojiano.

STORI: MWANDISHI WETU, IJUMAA