×

DUKA BOMBA: TEKNOLOJIA YA KITANZANIA YA KUDHIBITI MAUZO KWA NJIA YA SMS

Mara nyingi katika safu hii, tunajadili kuhusu teknolojia kubwa zilizovumbuliwa duniani, ambazo nyingi zinakuwa kwenye mataifa yaliyoendelea lakini kwa leo, tutajadili cha kwetu! Teknolojia mpya kabisa iliyovumbuliwa na Watanzania.

Wafanyabiashara wanaomiliki maduka, iwe ni makubwa au hata yale madogo ya mtaani, wana kawaida ya kuandika kila bidhaa zinazouzwa au zinazoingizwa dukani, ili iwe rahisi kujua mauzo ya siku, faida au hasara pale inapotokea.

Ni kawaida kabisa kwa wauzaji kuwa na madaftari makubwa dukani, kila kinachouzwa kinaandikwa kisha ndiyo unapewa risiti kama utahitaji. Kwa wale walioendelea na wenye mitaji mikubwa, wanakuwa na mifumo maalum ya kuhifadhi taarifa zote za mauzo kwenye kompyuta.

Ukinunua bidhaa, muuzaji anaingiza data kwenye kompyuta, kisha risiti inatoka. Hata hivyo, mifumo hii huwa ni ghali na inahitaji utaalamu na ujuzi wa kuiendesha kwa hiyo wafanyabiashara wengi, hawaimudu.

Kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana vijana wa Kitanzania wanaosoma ng’ambo, Paschal Giki na Said Hafidh Abdallah (Siderite) kupitia kampuni yao ya ubunifu wa mifumo ya kisasa, GIKI & SIDERITE CO. LTD wamekuja na teknolojia mpya iitwayo Duka Bomba.

 

 

Ni vijana hawahawa ndiyo waliovumbua mfumo wa kukata tiketi za mabasi kwa kutumia SMS za kawaida, ambapo unaweza kuchagua basi unalotaka kusafiria, ukachagua siti na kulipia ukiwa nyumbani kwako, kwa kutumia simu yako, tena siyo lazima iwe smartphone, hata ‘kitochi’.

Katika teknolojia hii ya Duka Bomba, muuzaji au mmiliki wa duka, anaweza kuhifadhi taarifa zake zote za mauzo na manunuzi kwa kutumia simu ya mkononi. Tena siyo ‘smartphone’, simu ya kitochi, isiyohitaji intaneti inatosha kabisa kufanya mambo yote ambayo pengine hujawahi kudhani kwamba yanawezekana.

Kinachofanyika katika teknolojia hii, muuzaji au mmiliki anajiandikisha kwenye ‘database’ kwa kutuma meseji ya kawaida, kisha anapewa maelekezo ya nini cha kufanya ili kufungua akaunti yake ya Duka Bomba. Ndani ya dakika tano tu, usajili unakuwa umeshakamilika.

Akishakamilisha usajili, akiwa hapohapo dukani kwake, atapewa jina maalum na namba ya siri, mfano Uwazi Shop 1234. Baada ya hapo, atakachokuwa anakifanya, kila bidhaa anayouza, anatuma meseji ya kawaida kwenda kwenye akaunti yake, akieleza ni bidhaa gani aliyouza, idadi na thamani.

Mfano, magazeti 2, 1800/= kwenda kwenye namba maalum aliyopewa wakati wa kujisajili. Mfumo utahifadhi kumbukumbu zote na mwisho wa wiki, akitaka kujua ameuza bidhaa zipi, kwa idadi ipi na gharama kiasi gani, atatuma meseji ya kawaida na ‘statement’ itaingia kwa kupitia meseji, ikimuonesha bidhaa zote alizouza na kiasi cha fedha zilizopatikana.

Pia atakuwa na uwezo wa kujua, amepata faida kiasi gani, kama kuna hasara itamuonesha ni kiasi gani na mfumo pia utamueleza ni bidhaa zipi anazotakiwa kwenda kuzileta dukani ili biashara iendelee! Simpo kabisa kwa kutumia meseji za kawaida tu.

Uzuri ni kwamba, unaweza kuona mwenendo wa mauzo dukani kwako, hata kama upo mbali na umemuajiri mtu dukani na kila mwisho wa mwezi, taarifa za mauzo kwa mwezi mzima zitakuwa zinakujia kupitia simu yako mahali popote ulipo.

Ukitaka kuprint ripoti ya mwezi mzima, utaelekezwa namna ya kufanya ambapo utaoneshwa mwenendo mzima wa biashara yako kwa mwezi mzima. Kwa mujibu wa wavumbuzi wa teknolojia hii, kila kitu kimeshakamilika na sasa wapo kwenye majaribio ya mwishomwisho na kukamilisha taratibu za kisheria kabla ya kuanza kuisambaza teknolojia hii nchi nzima, mijini mpaka vijijini. Unaweza kutembelea website yao kwa kubofya www.safaribomba.com.

Yajayo yanasisimua sana.