×

JENGO LA KAMPUNI LILILOGEUZWA DANGURO… OFM YATIBUA DILI!

BAADA ya hivi karibuni Kikosi cha Operesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kubaini ufuska mzito unaofanyika ndani ya jengo la kampuni lililopo maeneo ya Sinza Mori jijini Dar, dili limetibuka baada ya wamiliki wa jengo kufuta bango lililokuwepo getini kisha kuwapiga ‘biti’ wanawake waliokuwa wanajiuza katika eneo hilo.

Awali OFM ilitonywa kuwa, katika jengo hilo ndani hakuna biashara halali inayofanyika bali kuna vyumba kibao vinavyotumiwa na wanawake ambao wanafanya biashara ya ngono. Taarifa hizo hazikuwa mpya sana kwenye dawati la OFM kwani kuna wakati kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ilifanyika operesheni ya kulisafisha eneo hilo lililokubuhu kwa biashara ya uchangudoa.

Mbali na kelele nyingi za wananchi wa eneo hilo wakilalamikia uchafu unaofanyika ndani ya jengo hilo, wanawake hao pamoja na wamiliki wa jengo hilo waliendelea kuziba pamba masikioni hadi hivi karibuni OFM ilipotinga tena na kubaini kuwa, licha ya getini kuwepo na bango lililoandikwa ….Trading Co.LTD, ndani kuna ufuska unaofanyika.

Baada ya operesheni hiyo kisha OFM kuhakikisha taarifa inamfikia Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kupitia wasaidizi wake, dili lilitibuka ambapo lile bango lilifutwa siku gazeti lililoripoti habari hiyo la Ijumaa Wikienda lilipotoka huku ikidaiwa kuwa, hata wale mabinti waliokuwa wamepanga vyumba ndani ya jengo hilo wametimuliwa.

“Kwa kweli tunashukuru sana, baada ya kutoa ile habari, biashara imetibuka pale. Sasa hivi angalau pametulia na lile bango limefutwa. “Unajua ilikuwa ukipita pale na kuona lile bango unaamini kuwa kinachofanyika ndani ni halali, kumbe ufuska mtupu. OFM mmefanya kazi nzuri sana, endeleeni kufichua maovu,” alisema Sakina Juto wa Sinza Mapambano.

Naye mmoja wa vijana wanaofanya biashara pembeni kidogo na jengo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Sudi alisema: “Eneo hili limekuwa na usumbufu mkubwa sana, machangudoa walikuwa wengi, polisi wa doria wakipita usiku wanakimbia, baadaye wanarudi. Kuna siku wanakamatwa lakini wakiachiwa wanaingia tena barabarani ila sasa hivi mwenye jengo amekuwa mkali baada ya nyie kuandika.”

Eneo hilo linalotazamana na Kituo cha Mafuta cha Big Bon limekuwa maarufu sana kwa biashara ya ukahaba ambapo kila linapoingia giza, akinadada hasa wale waliojaaliwa maumbo makubwa hujipanga nje ya geti hilo kuwinda wateja, jambo ambalo limekuwa likileta usumbufu kwa wapita njia.

STORI: IGENGA MTATIRO, UWAZI